Na Mwandishi Wetu,
Dar es Salaam.
Wadau wa lishe nchini wameeleza kuwa matumizi ya vyakula visivyoongezwa virutubisho yanaendelea kuhatarisha afya za wananchi, hasa watoto na wanawake wajawazito, huku yakichangia kuongezeka kwa baadhi ya matatizo ya kuzaliwa nayo ikiwemo mgongo wazi na vichwa vikubwa.
Tahadhari hiyo imetolewa Juni 8, 2026 jijini Dar es Salaam katika Mkutano wa 40 wa Wadau wa Uongezaji Virutubisho Kwenye Vyakula, ambapo wadau mbalimbali walijadili hatua zinazochukuliwa kukabiliana na changamoto ya upungufu wa virutubisho nchini.
Akizungumza katika mkutano huo, Mkurugenzi wa Huduma za Lishe kutoka TAMISEMI, Luitfrid Nnally, alisema Serikali imeendelea kusimamia utekelezaji wa sheria na kutoa elimu kwa wazalishaji pamoja na wasindikaji wa vyakula ili kuhakikisha bidhaa zinazofika kwa walaji zina virutubisho vinavyohitajika.
Alisema uongezaji wa virutubisho kwenye vyakula ni moja ya mikakati muhimu ya kuzuia magonjwa yanayotokana na upungufu wa lishe, hususan kwa watoto na wanawake wajawazito.
“Tunawataka wote wanaojihusisha na biashara ya usindikaji wa vyakula kuhakikisha wanaongeza virutubisho kwenye bidhaa zao. Atakayebainika kukiuka sheria, hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi yake,” alisema Nnally.
Aidha, alibainisha kuwa bado kuna changamoto kwa baadhi ya wakulima wanaotumia mazao yao wenyewe, hususan mahindi, kutengeneza unga wa matumizi ya nyumbani bila kuongezwa virutubisho muhimu.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Taasisi ya Mwanangu Development Tanzania (MWADETA), Walter Miya, alisema taasisi hiyo inaendelea kutoa elimu kwa jamii kuhusu umuhimu wa lishe bora na namna ya kuwahudumia watoto wenye matatizo ya mgongo wazi na vichwa vikubwa.




Hakuna maoni: