WCF YAHIMIZA MATUMIZI YA TEKNOLOJIA KUIMARISHA HIFADHI YA JAMII

 WCF YASISITIZA TEKNOLOJIA KUIMARISHA HIFADHI YA JAMII NA UENDELEVU WA BIASHARA

Na Mwandishi Wetu

MFUKO wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF) umesisitiza umuhimu wa matumizi ya teknolojia na ushirikiano wa kimkakati katika kuimarisha mifumo ya hifadhi ya jamii, hatua itakayochochea ukuaji wa uchumi, kuongeza ajira na kupanua wigo wa wanachama.

Hayo yameelezwa na Mkuu wa Kitengo cha Takwimu na Hadhari wa WCF, James Tenga, alipokuwa akichangia katika mjadala wa kitaaluma ulioandaliwa na Chama cha Waajiri Tanzania (ATE), uliobeba mada isemayo, "Kuimarisha Hifadhi ya Jamii na Uendelevu wa Biashara kupitia Ushirikiano wa Kimkakati, Ufanisi wa Mifumo ya Udhibiti na Ushirikiano wa Taasisi."

Mjadala huo ulifanyika Juni 25, 2026 jijini Dar es Salaam, ukiwa sehemu ya Mkutano Mkuu wa Mwaka wa Waajiri ulioambatana na Kongamano la Waajiri, na uliwakutanisha wadau mbalimbali kutoka sekta ya ajira, hifadhi ya jamii na taasisi nyingine muhimu.

Tenga alisema kuwa utekelezaji mzuri wa mifumo ya kidijitali na miradi ya kimkakati kama Jamiinamba utasaidia kuongeza ufanisi katika utoaji wa huduma, kupanua wigo wa wanachama, kuongeza fursa za ajira na kuleta tija kwa mifuko ya hifadhi ya jamii, waajiri na wafanyakazi kwa ujumla.

Aliongeza kuwa ushirikiano wa karibu kati ya taasisi mbalimbali ni nguzo muhimu katika kujenga mfumo imara wa hifadhi ya jamii unaokidhi mahitaji ya soko la ajira na kuchangia maendeleo endelevu ya uchumi wa taifa.

Ushiriki wa WCF katika kongamano hilo umeendelea kuimarisha ushirikiano kati ya taasisi za hifadhi ya jamii, waajiri na wadau wengine muhimu, kwa lengo la kuboresha mazingira ya kazi, kuimarisha ulinzi wa wafanyakazi na kuhakikisha uendelevu wa shughuli rasmi za biashara nchini.

Hakuna maoni:

Inaendeshwa na Blogger.