DCEA, MKUU WA WILAYA YA TEMEKE WAHAMASISHA JAMII KUPAMBANA NA DAWA ZA KULEVYA

DAR ES SALAAM

Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA), kwa kushirikiana na Mkuu wa Wilaya ya Temeke, wameendesha tamasha maalum la kuhamasisha jamii kupinga matumizi na biashara ya dawa za kulevya, likiwa na lengo la kuongeza uelewa wa wananchi na kuimarisha ushiriki wa jamii katika vita dhidi ya tatizo hilo.

Akizungumza katika tamasha hilo, Mkuu wa Wilaya ya Temeke, Sixtus Mapunda, amesema kuchaguliwa kwa Temeke kuwa mwenyeji wa kampeni hiyo ni fursa muhimu kutokana na mazingira ya wilaya hiyo ambayo yanaweza kurahisisha usambazaji na matumizi ya dawa za kulevya.

Mapunda amesema mafanikio ya mapambano hayo yanategemea kukata ugavi wa dawa hizo pamoja na kupunguza uhitaji wake kupitia elimu kwa jamii. Amewataka wazazi kuzungumza na watoto wao mapema kuhusu madhara ya dawa za kulevya na kuwahimiza vijana kutokujaribu matumizi hayo kwa kuwa athari zake ni kubwa na mara nyingi ni vigumu kuzirekebisha.

Aidha, amewaonya vijana dhidi ya tamaa ya kuiga maisha ya kifahari yanayoonyeshwa kwenye mitandao ya kijamii bila kuwa na vyanzo halali vya kipato, akisema hali hiyo mara nyingi hutumiwa kuwashawishi kujiingiza katika biashara haramu ya dawa za kulevya au vitendo vya utakatishaji fedha.

Amewataka wananchi wa Temeke na Watanzania kwa ujumla kukataa dawa za kulevya kwa vitendo, huku akiwahimiza vijana kutumia muda wao kujenga maisha yenye tija na mustakabali bora.

Kwa upande wake, Kamishna Msaidizi wa DCEA, Dkt. Kasian Nyandindi, amesema mamlaka hiyo ina majukumu makuu manne katika mapambano dhidi ya dawa za kulevya, ambayo ni kuimarisha ukamataji wa dawa hizo na kuzuia usambazaji wake, kutoa elimu sahihi kwa umma, kuboresha huduma za tiba na utengamao kwa waraibu, pamoja na kuimarisha ushirikiano kuanzia ngazi ya jamii hadi kimataifa.

Dkt. Nyandindi amesema tatizo la dawa za kulevya linaathiri jamii nzima, hivyo linahitaji ushiriki wa kila mwananchi. Pia amewahimiza wananchi kutumia namba ya dharura 119 kutoa taarifa za wauzaji na wasambazaji wa dawa za kulevya ili kusaidia mamlaka kuchukua hatua dhidi ya wahalifu hao.

Katika tamasha hilo pia kulitolewa ushuhuda kutoka kwa baadhi ya waraibu waliopona, akiwemo Fatuma Mohammed, ambaye alieleza jinsi matumizi ya dawa za kulevya yalivyobadili maisha yake.

Fatuma amesema alijiingiza katika matumizi ya dawa za kulevya na baadaye kujikuta akifanya vitendo mbalimbali vya uhalifu na ukiukwaji wa maadili, ikiwemo kujiuza, kuiba na kukaba watu ili kupata fedha za kununua dawa hizo.

Amesema maisha yake yalianza kubadilika baada ya kupata msaada kupitia mashirika yanayoshirikiana na DCEA katika kutoa huduma za tiba, ushauri nasaha na utengamao kwa waraibu. Kwa sasa ameacha matumizi ya dawa za kulevya, ameanza upya maisha yake na anaendelea na shughuli halali za kujipatia kipato.

Fatuma amewataka vijana kujiepusha na matumizi ya dawa za kulevya, akisisitiza kuwa madhara yake ni makubwa na huathiri maisha ya mtu binafsi, familia na jamii kwa ujumla.

Tamasha hilo lilipambwa na michezo mbalimbali, ikiwemo mpira wa miguu na netiboli, ikiwa ni sehemu ya kuhamasisha ushiriki wa jamii katika kampeni za kupinga dawa za kulevya.


Hakuna maoni:

Inaendeshwa na Blogger.