Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) imebaini na kukamata makopo 122 ya vinywaji vya kuongeza nguvu (energy drinks) vyenye kemikali ya THC, inayopatikana kwenye dawa za kulevya aina ya bangi, katika operesheni iliyofanyika jijini Dar es Salaam.
Vinywaji hivyo vyenye chapa ya TRIP, vyenye ujazo wa mililita 250 kila kopo, sawa na lita 30.5, vilikamatwa baada ya DCEA kwa kushirikiana na Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali (GCLA), Shirika la Viwango Tanzania (TBS) na Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA) kufanya ukaguzi katika duka la Village Supermarket.
Akizungumza na waandishi wa habari Julai 02, 2026, Kamishna Jenerali wa DCEA, Aretas Lyimo, amesema katika operesheni hiyo watuhumiwa wawili, Syed Abdul Bast (43), raia wa Pakistan, na Dhirendra Kumar Gorodhan (45), Mtanzania mwenye asili ya Asia, walikamatwa na hatua za kisheria zinaendelea.
DCEA imeeleza kuwa kemikali ya THC inaweza kusababisha madhara mbalimbali kwa mtumiaji, ikiwemo kuamsha magonjwa ya akili, kubadili utendaji wa mfumo wa fahamu, kuchochea vitendo vya uhalifu na matumizi ya dawa nyingine za kulevya.
Hata hivyo, tukio hilo ni sehemu ya mafanikio ya operesheni zilizofanyika nchini kote kati ya Mei na Juni 2026, ambapo jumla ya tani 22.6 za dawa za kulevya, lita 30.5 na kilogramu 19.94 za dawa tiba zenye asili ya kulevya zilikamatwa.



Hakuna maoni: