Na Atley Kuni, WAF
Kasulu, Kigoma.
Serikali kupitia Wizara ya Afya kwa kushirikiana na CIHEB Tanzania chini ya Mradi wa Usalama wa Afya Duniani imeendelea kutoa elimu ya tahadhari ya dhidi ya Ebola kwa viongozi wa dini na watu mashuhuri katika Wilaya ya Kasulu, Mkoani Kigoma.
Elimu hiyo imetolewa leo Julai 23, 2026 ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuimarisha uelewa wa jamii na kuzuia uwezekano wa maambukizi na kuenea kwa ugonjwa huo ikiwa ni jitihada za serikali kuhakikisha maeneo ya mipakani hususan yale yanayopakana na nchi jirani zinazotajwa kuwa na ugonjwa wa Ebola yanatapata uelewa wa kutosha na namna ya kuchukua tahadhari.
Akizungumza wakati wa Mafunzo hayo Mratibu wa Elimu ya Afya kwa umma mkoa wa Kigoma Bw. Abeid Maichael amesema, mafunzo hayo yamelenga kuwajengea uwezo wa kuelewa dalili za Ebola, njia za maambukizi, namna ya kujikinga pamoja na hatua zinazopaswa kuchukuliwa endapo kutatokea mgonjwa anayeshukiwa.
"Viongozi wa dini na watu maarufu mnayo nafasi kubwa ya kuelimisha watu mlionao kupitia nyumba za ibada, huku watu maarufu wakitumia majukwaa yao na mikusanyiko mbalimbali kuhamasisha jamii kuzingatia hatua za kujikinga" amesema Dkt Abeid
Abeid amewataka viongozi hao kuendelea kufuata kanuni za usafi binafsi, kunawa mikono mara kwa mara, kuepuka kugusa majimaji ya mwili ya mtu mwenye dalili za ugonjwa huo na kutoa taarifa kwa mamlaka za afya mara moja endapo watabaini mtu mwenye dalili zinazofanana na Ebola.
Hatua hiyo inaelezwa kuwa ni sehemu ya mkakati wa kuimarisha utayari wa jamii dhidi ya Ebola kwa kuhakikisha elimu inawafikia wananchi kupitia viongozi wanaoaminika na wenye ushawishi katika maeneo yao.
Bw. Abeid amewataka Viongozi hao kuacha kula nyama au mizoga hususan za wanyama Pori kama Popo, Tumbili na Nyani ambao wanatajwa kama wanyama wenye ugonjwa huku akihimiza washiriki kuwa mabalozi wa elimu ya afya katika jamii na kusisitiza kuwa kinga ni bora kuliko tiba.









Hakuna maoni: