FEMA MINING YASISITIZA WATANZANIA KUSHIRIKI FURSA ZA SEKTA YA MADINI

Meneja wa Ununuzi wa kampuni ya FEMA Mining, Frank Joseph, amesema kampuni hiyo imefurahishwa kuwa mmoja wa wadhamini wa Jukwaa la Tano la Utekelezaji wa Ushirikishwaji wa Watanzania katika Sekta ya Madini (LCCF 2026), lililofanyika jijini Mwanza, ambapo imepata fursa ya kujifunza masuala mbalimbali ya ununuzi na namna Watanzania wanavyoweza kushiriki kikamilifu katika sekta ya madini.

Akizungumza na waandishi wa habari Julai 24, 2026, wakati wa kufungwa kwa jukwaa hilo, Joseph amewahimiza Watanzania kuendelea kushiriki katika majukwaa yanayowakutanisha wadau wa sekta ya madini ili kujifunza, kubadilishana uzoefu na kutumia fursa zinazopatikana katika sekta hiyo.

Amesema kampuni ya FEMA Mining inajishughulisha na shughuli za uchimbaji wa madini, ulipuzi wa miamba pamoja na ukodishaji wa vifaa vinavyorahisisha shughuli za uchimbaji migodini.

Aidha, amesema kampuni hiyo imeona fursa ya kushirikiana na makampuni kutoka nje ya nchi katika utekelezaji wa shughuli za madini, hatua ambayo inalenga kuongeza uwezo wa kampuni na kuchangia ukuaji wa uchumi.

Ameeleza kuwa FEMA Mining sasa imetimiza miaka mitano tangu kuanzishwa kwake, na katika kipindi hicho imechangia kuwawezesha vijana wengi kiuchumi kupitia ajira, na imeendelea kutekeleza wajibu wake kwa jamii (CSR) kwa kuhakikisha wananchi wanaozunguka migodi wananufaika kupitia fursa za ajira na miradi ya maendeleo, ikiwemo uchimbaji wa visima vya maji. 

Hakuna maoni:

Inaendeshwa na Blogger.