DAR ES SALAAM
Shirika la Kazi Duniani (International Labour Organization – ILO) nchini Tanzania limeadhimisha Siku ya Programu ya Start and Improve Your Business (SIYB) kwa Mara ya kwanza Dunia, huku likitoa wito kwa serikali, sekta binafsi na wadau wa maendeleo kuongeza uwekezaji katika programu hiyo ili kuwawezesha wajasiriamali kupata ujuzi, maarifa na fursa zitakazochochea ukuaji wa biashara, uzalishaji wa ajira na maendeleo ya uchumi.
Maadhimisho hayo, yaliyofanyika mapema hii leo Julai 17,2026, katika ofisi za ILO Jijini Dar es Salaam yalilenga kutathmini mafanikio ya programu ya SIYB pamoja na kujadili namna ya kuiimarisha ili iendane na mahitaji ya sasa ya biashara na maendeleo ya teknolojia.
Akizungumza katika maadhimisho hayo, Katibu Mtendaji wa Baraza la uwezeshaji wananchi kiuchumi NEEC Gwakisa Bapala amesema tangu kuanzishwa kwa programu hiyo nchini kupitia Youth Entrepreneurship Facility (YEF) mwaka 2010 hadi Julai 2026, zaidi ya wajasiriamali 70,000 wamepata mafunzo ya SIYB, huku programu hiyo ikichangia kuzalishwa kwa ajira mpya zaidi ya 15,000.
Pia amesema zaidi ya kampuni 50 zinazotoa Business Development Services (BDS) zimeendelea kushirikiana na programu hiyo katika kuwajengea uwezo wajasiriamali, hatua ambayo imeongeza upatikanaji wa huduma za ushauri na maendeleo ya biashara nchini.
"Kama Baraza, tunafanya kazi kwa karibu sana na ILO pamoja na wadau mbalimbali, ikiwemo Chama cha SIYB Afrika Mashariki (SIYB East Africa Association), kuhakikisha nguzo ya stadi na maarifa inaendelea kuimarishwa. Kwa sasa Tanzania ina wakufunzi zaidi ya 336 wa SIYB, Wakufunzi Wakuu saba (Master Trainers) pamoja na Mtengenezaji mmoja wa Wakufunzi Wakuu (Master Trainer Developer)," alisema.
Aidha, alisema programu ya SIYB imeanza kufanya mageuzi ya kidijitali kwa kuhamishia sehemu ya mafunzo yake kwenye mifumo ya mtandao na kuimarisha matumizi ya masoko ya kidijitali. Hatua hiyo inalenga kuwasaidia wajasiriamali wa Biashara Ndogo na za Kati (Small and Medium Enterprises – SMEs) kutumia teknolojia za kisasa, ikiwemo Akili Mnemba (Artificial Intelligence – AI), katika kufanya tafiti za masoko, kubuni vifaa vya matangazo na kuandaa taarifa za kifedha kwa ufanisi zaidi.
Akizungumza wakati akichangia mada katika maadhimisho hayo mtaalamu wa maswala ya AI Dkt. Denis Mwigusa Alitoa tahadhari kuhusu matumizi ya AI bila usimamizi wa kibinadamu, akisema matumizi ya teknolojia hiyo yanapaswa kuambatana na uhakiki na maboresho ya kitaalamu.
Alibainisha kuwa baadhi ya maandiko ya biashara na kitaaluma yamekuwa yakikataliwa kutokana na kutegemea AI kwa asilimia mia moja bila kuyafanyia marekebisho yanayohitajika.
Aidha alisema kuwa AI imekuja kurahisha shughuli za kibinadamu ambapo waru wa kawaida wanaweza kutumia kufanyashughuli zao kutengeneza mabango,kuandaa ripoti za mwaka ama robo mwaka kwa kutumia Ai na baadae kuhakikiwa na Binadamu.
Kwa upande wake, Mwakilishi wa Mkurugenzi Mkazi wa ILO Dkt. Anna marie nchini alitoa wito kwa serikali na sekta binafsi kuendelea kuwekeza katika programu ya SIYB, akisisitiza kuwa biashara zinazowekeza kwa wafanyakazi wake, kuheshimu haki za msingi za kazi na kuendeshwa kwa uwajibikaji ndizo msingi wa uchumi imara na maendeleo endelevu ya kijamii na kiuchumi.
Aliongeza kuwa ILO huendelea kufanya tathmini na maboresho ya mtaala wa SIYB kila baada ya miaka mitano kupitia utafiti maalumu unaojulikana kama Tracer Study, unaoshirikisha wataalamu wa kimataifa ili kuhakikisha mafunzo yanayotolewa yanaendana na mahitaji ya soko, maendeleo ya teknolojia na mazingira ya sasa ya biashara.
Maadhimisho hayo yamefanyika wakati maandalizi yakiendelea kwa Mkutano wa Kimataifa wa AI na Mustakabali wa Kazi (International Conference on AI and Future of Work) unaotarajiwa kufanyika mwezi Septemba mwaka huu, ambapo matumizi ya teknolojia katika dunia ya kazi yanatarajiwa kuwa miongoni mwa ajenda kuu.

Hakuna maoni: