Na Mwandishi Wetu,
Dar es Salaam.
Bodi ya Ithibati ya Waandishi wa Habari (JAB) imezindua rasmi Mwongozo wa Kisheria wa Utoaji wa Ithibati ya Maisha kwa Waandishi wa Habari Wakongwe, hatua inayolenga kutambua na kuthamini mchango wa waandishi waliolitumikia taifa kwa miaka mingi kabla ya kuanzishwa kwa mfumo wa sasa wa ithibati.
Hotuba ya Mwenyekiti wa Bodi ya Ithibati ya Waandishi wa Habari, Bw. Tido Mhando, ilisomwa kwa niaba yake na Dkt. Egbert Mkoko wakati wa maadhimisho ya JAB Day yaliyofanyika katika Maonesho ya 50 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (Sabasaba).
Katika hotuba hiyo, Mhando alisema maadhimisho hayo ni fursa ya kuisogeza JAB karibu na waandishi wa habari pamoja na wananchi, huku akiipongeza Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo kwa kuendelea kuzipa taasisi zake nafasi ya kujitambulisha kupitia maonesho hayo, jambo ambalo limeongeza uelewa wa wananchi kuhusu majukumu ya taasisi za wizara na kuimarisha ushirikiano kati ya serikali na wadau wa sekta ya habari.
Amesema katika kipindi cha mwaka mmoja tangu Bodi hiyo ianze rasmi kutekeleza majukumu yake, imepokea maombi 4,521 ya ithibati, ambapo maombi 3,658 yameidhinishwa, 301 yanaendelea kufanyiwa kazi, 140 yamekataliwa kutokana na kutokidhi vigezo vilivyowekwa, huku maombi 422 yakisubiri kukamilishwa kwa nyaraka na taarifa zinazohitajika.
Aidha, amesema Bodi imeendelea kutoa elimu kwa wadau mbalimbali na kuimarisha ushirikiano na vyuo vikuu, vyuo vya kati, Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote, Idara ya Habari–MAELEZO, Jeshi la Polisi Tanzania pamoja na vyombo vya habari, hatua iliyosaidia kuhamasisha uzingatiaji wa maadili, weledi na utekelezaji wa Sheria ya Huduma za Habari nchini.
Mhando amesema moja ya maeneo yaliyoibua mjadala mkubwa kutoka kwa wadau ni namna ya kutambua mchango wa waandishi wa habari wakongwe waliotoa huduma kubwa kwa taifa kabla ya kuwepo kwa mfumo wa sasa wa ithibati na masharti ya kitaaluma yaliyowekwa na sheria.
Ameeleza kuwa kutokana na mabadiliko ya teknolojia na ukuaji wa sekta ya habari, Serikali iliianzisha JAB kwa jukumu la kusimamia taaluma ya uandishi wa habari, kutoa ithibati kwa waandishi, kusimamia maadili ya taaluma, kuandaa mafunzo na kuhakikisha sekta hiyo inaendelea kujengwa katika misingi ya weledi na uwajibikaji.
Kwa mujibu wa hotuba hiyo, historia ya taaluma ya habari nchini imejengwa na kizazi cha waandishi waliotoa mchango mkubwa katika kuhabarisha umma na maendeleo ya taifa, lakini baadhi yao hawakupata nafasi ya kujiendeleza kielimu ili kukidhi vigezo vya mfumo wa sasa wa ithibati. Kutokana na hali hiyo, Sheria na Kanuni zimetoa mamlaka kwa Bodi kutoa Ithibati ya Maisha kwa watu wenye utumishi uliotukuka na mchango wa kipekee katika sekta ya habari.
Amesema mwongozo mpya umeweka utaratibu wa utekelezaji wa mamlaka hayo kwa uwazi na kwa kuzingatia sheria, huku ukibainisha masharti ya waombaji ikiwemo kuwa raia wa Tanzania, kuwa na historia ya kazi za kihabari, ushahidi wa uzoefu na mchango katika taaluma, kuwa na elimu ya angalau stashahada katika taaluma inayotambulika na kutokuwa na rekodi ya ukiukaji wa maadili ya taaluma ya habari.
Aidha, amesema kuhusu kigezo cha umri, Bodi imezingatia masharti ya kipindi cha mpito cha Sheria ya Huduma za Habari ya mwaka 2016, ambapo waombaji wanaostahili kunufaika na utaratibu huo ni wale waliokuwa na umri wa angalau miaka 50 mwaka 2016, wakizingatiwa kuwa walikuwa tayari wamejijengea uzoefu mkubwa katika taaluma hiyo.
Mhando amesisitiza kuwa utoaji wa Ithibati ya Maisha hautafanyika kwa misingi ya upendeleo, bali kila ombi litafanyiwa tathmini kwa kuzingatia ushahidi, Sheria ya Huduma za Habari na Kanuni zake ili kulinda hadhi, maadili na weledi wa taaluma ya uandishi wa habari nchini.
Akihitimisha hotuba yake, aliwapongeza waandishi wa habari kwa mchango wao katika maendeleo ya taifa na kutangaza rasmi kuanza kutumika kwa Mwongozo wa Kisheria wa Utoaji wa Ithibati ya Maisha kwa Waandishi wa Habari Wakongwe, akieleza kuwa hatua hiyo itasaidia kuimarisha taaluma ya habari kwa kutambua mchango wa waandishi wakongwe huku ikilinda viwango vya taaluma kwa vizazi vya sasa na vijavyo.


Hakuna maoni: