Dar es Salaam.
Serikali kupitia Wizara ya Katiba na Sheria imeendelea kuhamasisha matumizi ya njia mbadala za utatuzi wa migogoro (ADR), ikieleza kuwa usuluhishi hutoa fursa kwa pande zinazohusika kufikia mwafaka kwa amani na kuridhika, tofauti na mashauri ya mahakamani ambayo mara nyingi huishia upande mmoja kushinda na mwingine kushindwa.
Kauli hiyo imetolewa na Naibu Waziri wa Katiba na Sheria, Mheshimiwa Zainab Athuman Katimba, alipotembelea mabanda ya taasisi zilizo chini ya wizara hiyo katika Maonesho ya 50 ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam (Sabasaba), Julai 1, 2026. Akiwa kwenye banda la wizara, pia alishiriki kutoa huduma za msaada wa kisheria kwa wananchi.
Katimba amesema licha ya Mahakama kubaki mhimili mkuu wa utoaji wa haki nchini, Serikali inaona umuhimu wa kuendeleza matumizi ya usuluhishi na njia nyingine mbadala za kutatua migogoro ili kuimarisha maridhiano na kupunguza migongano katika jamii.
Ameeleza kuwa wananchi wanaofika kupata msaada wa kisheria hupewa elimu kuhusu uwepo wa njia hizo, ambazo mara nyingi hutoa suluhisho la kudumu na linalokubalika kwa pande zote zinazohusika.
Katika ziara hiyo, Katimba pia alitembelea banda la Tume ya Marekebisho ya Sheria na kusisitiza umuhimu wa kuendelea kufanya mapitio ya sheria ili ziweze kuendana na utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, ambayo imeanza kutekelezwa katika mwaka wa fedha 2026/27.
Amesema mafanikio ya Dira 2050 yatahitaji mfumo wa sheria unaokwenda sambamba na mageuzi ya kiuchumi, kijamii na kiteknolojia yanayotarajiwa katika kipindi hicho.
Aidha, amesisitiza kuwa ukuaji wa teknolojia na mwelekeo wa uchumi wa kidijitali unaifanya Tanzania kuhitaji sheria zinazowezesha matumizi ya mifumo ya kisasa, ikiwemo kuelekea uchumi usiotegemea fedha taslimu.
"Ni muhimu sheria zetu zikawa za kisasa na ziendane na maendeleo ya teknolojia ili ziweze kuhimili mabadiliko ya dunia na kusaidia utekelezaji wa sera pamoja na mipango ya maendeleo," amesema.
Katimba pia alitembelea banda la Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, ambapo ameipongeza kwa kuendelea kutoa elimu kwa wananchi kuhusu haki za binadamu na kupokea maoni pamoja na changamoto mbalimbali.
Hata hivyo, ameisisitiza tume hiyo kuendelea kutoa elimu inayoweka msisitizo si tu kwenye haki za binadamu, bali pia wajibu wa kila mwananchi wa kuheshimu na kulinda haki za wengine.
Amefafanua kuwa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inaeleza wazi kuwa matumizi ya haki za mtu mmoja hayawezi kuvuka mipaka na kuathiri haki za wengine, huku kila mwananchi akiwa na wajibu wa kuheshimu sheria na kulinda maslahi ya taifa.
Kwa mujibu wa Katimba, uelewa wa uwiano kati ya haki na wajibu utasaidia kujenga jamii inayozingatia utawala wa sheria, kuheshimiana na kudumisha amani, ambayo ni msingi muhimu wa maendeleo endelevu ya taifa.


Hakuna maoni: