KMK ZANZIBAR ARDHIA KUWA BALOZI NA MKT MPYA WA BIMA TANZANIA

 


 ZANZIBAR. 

Katibu wa Baraza la Mapinduzi na Katibu Mkuu Kiongozi Zanzibar Bi Mansura Mosi Kassim ameridhia ombi la Kamishna wa Bima Dkt. Baghayo Saqware kuwa  Balozi wa Bima na pia Mkt. wa mabalozi wa bima nchini.

Hayo yamejiri wakati Kamishna wa Bima pamoja na baadhi ya wajumbe kutoka TIRA walipozuru ofisini kwa Kiongozi huyo Julai 1, 2026 ambapo pamoja na maswala mengine Kamishna wa Bima alimpongeza kwa kuteuliwa na Rais wa Zanzibar na Mkt. wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi kushika wadhifa huo.

Bi Mansura Kassim anachukua nafasi ya Mhandisi Zena aliyekuwa Mkt. wa Mabalozi wa Bima ambae kwa sasa ni Balozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Saudi Arabia.

Akitoa maneno mafupi mara baada ya kukubali ombi la kuwa Mkt. na Balozi wa Bima nchini Bi Mansura ameipongeza TIRA na sekta ya bima kwa ujumla kwa dhamira ya kuwafikia wananchi kupitia mbinu mbalimbali ikiwemo hii ya mabalozi wa bima na kuwataka kuongeza juhudi kuwafikia wananchi wengi zaidi hasa vijijini huku akisisitiza pia kuhusu sekta ya bima kuwa chanzo cha ajira kwa vijana.

Awali Dkt. Saqware kwenye maneno yake ya utangulizi alimweleza Katibu Mkuu Kiongozi juu ya majukumu yanayofanywa na mabalozi wa bima katika kusaidia kukuza sekta ya bima nchini kwa kusaidia kupeleka uelewa wa maswala muhimu ya bima kwa viongozi wenzao ambao ndiyo sauti kwa jamii wanazoziongoza.

“Kwa umuhimu wa sekta ya bima kwenye kukabiliana na majanga ni vyema kila mwanachi kuweza kukinga mali na afya hivyo ni vyema pia swala hili likaeleweka vizuri kwa wananchi wote. Sisi kama TIRA tunatumia njia mbalimbali kupitia vyombo vya Habari, mikutano ya hadhara, maoonesho lakini pia kupitia Mabalozi wa Bima” alisema Dkt. Saqware.

TIRA inaungana na sekta ya bima kwa ujumla kumshukuru Mkt. mpya wa Mabalozi na kumkaribisha kuungana na Mabalozi wengine kuendelea kuimarisha sekta ya bima nchini.

 

TIRA kwa soko salama la bima.

Hakuna maoni:

Inaendeshwa na Blogger.