MADINI YA YODERITE YATAKIWA KUHIFADHIWA KWA MANUFAA YA VIZAZI VIJAVYO

Dodoma – Kongwa.

Imeelezwa kuwa kuna umuhimu wa kuchukua hatua madhubuti za kuhifadhi na kulinda madini adimu aina ya Yoderite yanayopatikana katika eneo la Mlima wa Mautia, Wilaya ya Kongwa, Mkoa wa Dodoma, ili kuhakikisha urithi huo wa kipekee wa kijiolojia unabaki salama kwa manufaa ya vizazi vya sasa na vijavyo.

Hayo yalisemwa Juni 30, 2026 na Meneja wa Jiolojia kutoka Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST), Solomon Maswi, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari waliotembelea eneo hilo kwa ziara maalumu.

Maswi alisema kuwa uhifadhi wa Yoderite unaweza kuiwezesha Tanzania kuwa kitovu cha kimataifa cha tafiti kuhusu madini adimu, sambamba na kuongeza idadi ya watalii wanaotembelea maeneo yenye urithi wa jiolojia.

Aliongeza kuwa Yoderite ni miongoni mwa madini adimu yanayoifanya Tanzania kutambulika duniani kutokana na historia yake ya kugunduliwa kwa mara ya kwanza katika Mlima wa Mautia.

Aidha, alifafanua kuwa madini hayo yana mchango mkubwa katika tafiti za kisayansi kwa kusaidia kuelewa mchakato wa uundaji wa miamba na mazingira yenye shinikizo na joto la juu ndani ya ganda la dunia. Pia yana umuhimu mkubwa katika elimu ya jiolojia, maendeleo ya utalii wa jiolojia na uhifadhi wa urithi wa asili duniani.

Maswi alibainisha kuwa, kutokana na uchache wake na kupatikana katika maeneo machache sana duniani, madini ya Yoderite hayachimbwi kwa matumizi ya viwandani wala biashara. Badala yake, yanahifadhiwa kama urithi wa kipekee wa kijiolojia unaovutia watafiti, wanafunzi, wataalamu wa sayansi na watalii kutoka ndani na nje ya nchi. Hali hiyo inaipa Tanzania fursa ya kujijengea hadhi kama kitovu cha tafiti za kimataifa na utalii wa jiolojia unaotegemea urithi wa asili.

Taasisi za utafiti wa madini na vyuo vya Madini vimeshauriwa kutumia eneo hilo kwa mafunzo endelevu ya utafiti wa madini.

Madini ya Yoderite yaligunduliwa kwa mara ya kwanza duniani mwaka 1959 katika Milima ya Mautia, Wilaya ya Kongwa, Mkoa wa Dodoma.

Kutokana na kuendelea kwa tafiti baada ya miaka 35 watafiti wa miamba na madini walifanikiwa kugundua aina hiyo ya madini nchini Zimbambwe.

Jina la Yoderite lilipewa kwa heshima ya mwanajiolojia mashuhuri wa Marekani, Hatten Yoder Jr., kutokana na mchango wake mkubwa katika tafiti za miamba na madini.

Hakuna maoni:

Inaendeshwa na Blogger.