MAKUMBUSHO YA TAIFA LA TANZANIA YAENDELEA KUTANGAZA URITHI WA TAIFA KUPITIA KONGAMANO LA KIMATAIFA LA KISWAHILI NCHINI UFARANSA

Makumbusho ya Taifa la Tanzania inaendelea kuutangaza na kuhamasisha urithi wa Taifa katika ngazi ya kimataifa kupitia ushiriki wake katika Kongamano la Kimataifa la Kiswahili, lililofanyika kuanzia tarehe 4 hadi 7 Julai 2026 jijini Paris, nchini Ufaransa.

Kama taasisi yenye dhamana ya kuhifadhi, kulinda, kufanya tafiti na kuendeleza urithi wa asili na utamaduni wa Tanzania, Makumbusho ya Taifa la Tanzania imetumia kongamano hilo kuonesha nafasi muhimu ya lugha ya Kiswahili kama sehemu ya utambulisho wa Taifa, urithi wa kitamaduni na nyenzo muhimu ya kuhifadhi na kuendeleza historia, mila na desturi za Watanzania katika jukwaa la kimataifa.

Kupitia ushiriki huo, Makumbusho ya Taifa la Tanzania imeendelea kusisitiza mchango wake katika kuhamasisha matumizi ya Kiswahili kama chombo cha kuhifadhi na kurithisha maarifa ya kizazi hadi kizazi, sambamba na kuitangaza Tanzania kama kitovu cha urithi wa Kiswahili duniani.

Katika kongamano hilo, Makumbusho ya Taifa la Tanzania imewakilishwa na Bi. Wilhemina Deogratious Joseph, Mhifadhi Mwandamizi wa Kijiji cha Makumbusho (Senior Curator), ambaye ameshiriki katika mijadala na shughuli mbalimbali zilizolenga kuimarisha nafasi ya lugha ya Kiswahili na urithi wa kitamaduni katika maendeleo ya jamii na ushirikiano wa kimataifa.

Hakuna maoni:

Inaendeshwa na Blogger.