Na Mwandishi Wetu,
Dar es Salaam.
Makamu Mwenyekiti wa ACT Wazalendo Tanzania Bara, Isihaka Mchinjita, amesema tamko la maridhiano ya kisiasa kati ya ACT Wazalendo na CCM kwa upande wa Zanzibar limefikiwa baada ya takribani miezi minane ya mazungumzo yaliyofanyika kufuatia mvutano wa kisiasa ulioibuka baada ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2025.
Mchinjita amesema kabla ya kufikiwa kwa maridhiano hayo, ACT Wazalendo ilisimama imara kutoshiriki Serikali ya Umoja wa Kitaifa hadi pale mazingira yatakapowekwa ili kuhakikisha serikali hiyo inatekeleza madhumuni yaliyokusudiwa na Katiba ya Zanzibar.
Amesema kutokana na maswali na tafsiri mbalimbali zilizojitokeza kuhusu tamko hilo, chama kimeona ni muhimu kutoa ufafanuzi kwa wananchi, wadau wa demokrasia na Watanzania kwa ujumla kuhusu maana ya hatua hiyo na msimamo wake.
"Tamko hili linahusu mahsusi mchakato wa maridhiano ya kisiasa Zanzibar. Ndiyo maana tunaona ni muhimu wananchi wapate uelewa sahihi kuhusu kilichofikiwa na msimamo wa ACT Wazalendo," amesema Mchinjita.
Ameeleza kuwa Tanzania ni Jamhuri ya Muungano inayoundwa na Tanzania Bara na Zanzibar, huku akisisitiza kuwa historia na mazingira ya kisiasa ya Zanzibar yanatofautiana kwa kiasi kikubwa na yale ya Tanzania Bara.
Kwa mujibu wa Mchinjita, Zanzibar imepitia hatua mbalimbali za kisiasa tangu mwaka 1995, hivyo suluhisho la changamoto zake linapaswa kuzingatia historia hiyo ya muda mrefu.
Aidha, amesema mbali na CCM, ACT Wazalendo ni miongoni mwa vyama vyenye ushawishi mkubwa Zanzibar na pia kina uwepo Tanzania Bara, jambo linalokipa nafasi ya kuelewa kwa undani historia na mwelekeo wa siasa za Zanzibar.
Amedai kuwa katika mazingira ya uchaguzi huru na wa haki, ACT Wazalendo imekuwa ikifanya vizuri Zanzibar, ikiwemo kushinda viti vya udiwani na ubunge katika maeneo mbalimbali ya Pemba na Unguja.
Mchinjita pia amesema ACT Wazalendo kimerithi harakati za kisiasa zilizokuwa zikiongozwa na Chama cha Wananchi (CUF) chini ya hayati Maalim Seif Sharif Hamad, hali inayokifanya kuwa sehemu ya historia ya mapambano ya demokrasia Zanzibar tangu mwaka 1995.
Amesisitiza kuwa uzoefu huo unakiwezesha chama kutafsiri kwa usahihi hali ya kisiasa ya Zanzibar na kushiriki katika kutafuta suluhisho la kudumu la changamoto zinazoikabili Zanzibar.

Hakuna maoni: