DAR ES SALAAM.
Hospitali ya Medinova Specialized Polyclinic, inayomilikiwa na kampuni ya 33 Holding kutoka Qatar, imezindua rasmi Idara ya Tibamazoezi (Physiotherapy) ikiwa ni sehemu ya mkakati wake wa kupanua huduma za kibingwa na kuboresha upatikanaji wa huduma za afya nchini.
Dkt. Bwaja aliishukuru Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuweka mazingira mazuri ya uwekezaji katika sekta ya afya, huku akitoa shukrani kwa viongozi wa Mkoa wa Dar es Salaam na Wilaya kwa ushirikiano wanaoendelea kuipatia hospitali hiyo.
Alieleza kuwa bado jamii ina dhana potofu kuhusu huduma hiyo, akifafanua kuwa tofauti na massage ambayo hutoa nafuu ya muda mfupi, tibamazoezi hulenga kubaini chanzo cha tatizo na kutoa suluhisho la muda mrefu kupitia mazoezi maalumu, tiba kwa kutumia mikono (Manual Therapy) pamoja na vifaa vya kisasa vya umeme (Electrotherapy).
Dkt. Mpiri alisema huduma hiyo si kwa watu waliopata ajali au kufanyiwa upasuaji pekee, bali pia huwasaidia wagonjwa wenye matatizo ya mfumo wa upumuaji, mfumo wa fahamu, kizunguzungu, pamoja na kuimarisha misuli ya nyonga kwa ajili ya kudhibiti mkojo na kupunguza maambukizi ya mara kwa mara ya njia ya mkojo.
Aidha, aliwataka wananchi kuepuka kuiga mazoezi ya tibamazoezi yanayopatikana mtandaoni bila ushauri wa mtaalamu, akieleza kuwa kila mgonjwa hupangiwa mazoezi kulingana na umri, jinsia, hali ya afya na mahitaji yake binafsi.
Aliongeza kuwa tiba hiyo haihusishi maumivu makali kama wengi wanavyodhani na mara nyingi huhitaji vipindi kadhaa vya matibabu ili kuusaidia mwili na mfumo wa fahamu kurejesha uwezo wa kufanya kazi ipasavyo.
Alitaja baadhi ya matatizo yanayotibiwa kuwa ni pamoja na maumivu ya mgongo, shingo, magoti, matatizo ya misuli na mifupa, changamoto zinazotokana na ajali na kuvunjika mifupa, pamoja na matatizo ya mfumo wa fahamu ikiwemo wagonjwa wa kiharusi (stroke).
PT Lema alisema takwimu za dunia zinaonesha mahitaji ya huduma za tibamazoezi yanaongezeka kwa kasi kwa watu wa rika zote kutokana na ongezeko la magonjwa na changamoto zinazopunguza uwezo wa watu kutekeleza shughuli zao za kila siku.
"Idara hii imekuja kama suluhisho la kuwasaidia wananchi kurejesha uwezo wao wa kufanya shughuli za kila siku kwa ufanisi na kuboresha ubora wa maisha yao," alisema.
Alifafanua kuwa matibabu hayo hutolewa kupitia njia mbili kuu ambazo ni Manual Therapy, ambapo mtaalamu hutumia mikono kutoa matibabu, na Electrotherapy, inayohusisha matumizi ya vifaa maalumu vya kisasa vya tiba.
Mbali na huduma za tibamazoezi, Medinova pia hutoa huduma za kibingwa za magonjwa ya ndani, watoto, afya ya wanawake, magonjwa ya ngozi na urembo, afya ya kinywa na meno kupitia madaktari bingwa mbalimbali, pamoja na maabara ya kisasa inayotoa majibu ya haraka na yenye uhakika.
PT Lema alihitimisha kwa kuwakaribisha wananchi kufika Medinova Specialized Polyclinic kupata huduma za tibamazoezi na huduma nyingine za kibingwa kwa lengo la kuboresha afya na kurejesha uwezo wa mwili kufanya kazi kwa ufanisi.
Aidha, hospitali hiyo imeeleza kuwa inaendelea na mipango ya kupanua miundombinu yake, ikiwemo kuongeza uwezo wa huduma za kulaza wagonjwa na kuanzisha huduma za dharura, kwa lengo la kuwahudumia wananchi wengi zaidi kwa ufanisi.











Hakuna maoni: