MRADI WA KILIMO ENDELEVU WAONDOA MIKOPO 'KAUSHA DAMU'

MRADI WA KILIMO ENDELEVU WAONDOLEA WAKULIMA MIKOPO ‘KAUSHA DAMU’

Na Mwandishi Wetu, 

Arusha

Mradi wa Kilimo Endelevu unaotekelezwa katika vijiji vya Seuri na Oldonyowas mkoani Arusha umeleta matumaini mapya kwa wakulima kwa kuwaepusha na mikopo yenye masharti magumu maarufu kama 'kausha damu'.

Mradi huo unafadhiliwa na Shirika la Island of Peace (IDP) kwa kushirikiana na Shirika la Utafiti, Ushauri wa Kitaalamu na Miradi ya Maendeleo ya Jamii (RECODA), na umewanufaisha zaidi ya wakulima 700 kutoka vijiji 10.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti na mwandishi wa habari hizi, baadhi ya wakulima wamesema walikuwa wamekata tamaa ya kuendelea na kilimo kutokana na mavuno duni, lakini tangu kuanza kwa mradi huo wameanza kushuhudia mabadiliko makubwa katika uzalishaji na kipato.

Mkulima wa kijiji cha Seuri, Witness Sikoi, amesema IDP na RECODA vimemrejeshea imani kwamba kilimo kinaweza kuwa chanzo cha maendeleo kutokana na mafanikio aliyoyapata.

Witness, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kikundi cha Elishorie, amesema kabla ya kuanza kwa mradi huo wanawake wengi walitegemea mikopo yenye masharti magumu iliyosababisha migogoro katika familia.

"Hatukuwa na amani kutokana na mikopo ya kausha damu, lakini sasa tunaishi kwa utulivu. Tunalima eneo dogo, tunapata mavuno mengi na soko la uhakika," amesema.

Ameongeza kuwa kupitia vikundi vya kuweka na kukopa walivyoanzisha, wanapata mitaji ya kuendesha shughuli zao bila kutegemea mikopo yenye riba kubwa.

Kwa upande wake, Neema Augustino wa Kikundi cha Faida amesema mradi huo umewapa elimu ya kilimo ikolojia, kinacholinda mazingira huku kikiongeza uzalishaji na kipato.

"Mradi wa Kilimo Endelevu umeniwezesha kupanda ndizi, kufuga nguruwe na kujiunga na vikoba, jambo linalonihakikishia maisha bora ya baadaye," amesema.

Neema amesema pia mradi huo umeongeza ushirikiano kati ya wanandoa katika shughuli za uzalishaji, tofauti na ilivyokuwa hapo awali.

Mwalimu wa wakulima hao, Richard Kivuyo, amesema ushirikiano mkubwa kutoka kwa wanufaika umeifanya kazi ya kutoa mafunzo kuwa rahisi na yenye matokeo mazuri.

Naye mkulima wa mbogamboga kutoka Oldonyowas, Flora Molel, amesema kilimo ikolojia kina faida nyingi kiuchumi, kijamii na kiafya.

Amesema hulima bilinganya, sukuma wiki, spinachi, saro, mnavu na mboga nyingine kwa kutumia mbinu za kilimo ikolojia.

"Mazao yangu yana soko la uhakika, na pia nauza kupitia mtandao, jambo linaloniwezesha kupata kipato cha uhakika," amesema.

Flora amesema mafanikio hayo yamemfanya kutambulika kitaifa baada ya kuibuka mshindi wa kwanza wa kilimo ikolojia katika Wilaya ya Arusha mwaka jana.

Mkurugenzi Mkuu wa RECODA, Josephine Ng'ang'a, amesema mradi huo umeonyesha mafanikio makubwa, huku baadhi ya vikundi vya wakulima vikizalisha vikundi vingine kupitia uzoefu walioupata.

Amesema RECODA imeendelea kushirikiana na Serikali kutekeleza miradi ya maendeleo kwa kuzingatia misingi ya RIPAT yenye kaulimbiu isemayo, "Njaa na Umasikini Inawezekana Kuwa Historia."

Hakuna maoni:

Inaendeshwa na Blogger.