POLISI WABAINI NJAMA ZA VURUGU, WATOA ONYO KALI KABLA YA SABASABA

DAR ES SALAAM. 

Jeshi la Polisi Tanzania limefichua kile ilichokieleza kuwa ni mipango ya siri ya vikundi vya watu wachache wanaotumia mitandao ya kijamii kuhamasisha vurugu, kushambulia viongozi na wananchi, pamoja na kupanga mashambulizi dhidi ya askari kwa lengo la kupora silaha na kuvuruga amani ya nchi.

Katika taarifa rasmi iliyotolewa leo, Jumapili Julai 5, 2026, Msemaji wa Jeshi la Polisi, David Misime, amesema tayari baadhi ya watu wanaodaiwa kuhusika na uratibu wa mipango hiyo wamekamatwa huku uchunguzi ukiendelea ili kuwafikisha mahakamani.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, uchunguzi umebaini kuwa baadhi ya watu wamekuwa wakitumia mitandao ya kijamii na majukwaa ya majadiliano mtandaoni kuhamasishana kutekeleza vitendo vya vurugu, ikiwemo kushambulia viongozi, kuchoma shule, kuharibu na kupora mali za umma na binafsi, pamoja na kushambulia askari ili kupora silaha.

Polisi imesema baadhi ya wahusika wamekuwa wakitumia hoja ya haki ya kuandamana kama kisingizio cha kutekeleza vitendo hivyo, huku ikisisitiza kuwa maandamano hayo hayajafuata taratibu za kisheria na kiusalama zinazotakiwa.

Aidha, Jeshi la Polisi limeonya kuwa halitavumilia mtu au kikundi chochote kitakachojihusisha na mipango hiyo na kwamba hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi ya wote watakaobainika kuhusika.

Pamoja na tahadhari hiyo, Jeshi la Polisi limewahakikishia Watanzania kuwa hali ya usalama nchini inaendelea kuwa shwari na kwamba, kwa kushirikiana na vyombo vingine vya ulinzi na usalama, limeimarisha doria na ulinzi katika maeneo mbalimbali ya nchi kuelekea maadhimisho ya Sabasaba.

Jeshi hilo pia limesema ulinzi utaimarishwa zaidi katika Maonesho ya 50 ya Biashara ya Kimataifa yanayofanyika katika Viwanja vya Sabasaba, Barabara ya Kilwa, jijini Dar es Salaam, ili kuhakikisha usalama wa washiriki na wananchi wote.

Hakuna maoni:

Inaendeshwa na Blogger.