Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera Bunge Uratibu na wenye Ulemavu Profesa Palamagamba Kabudi ameanza ziara ya siku tatu katika Mkoa wa Dar es Salaam ambapo leo Julai 19,2026 amezindua mitambo ya ujenzi wa miundombinu Wilaya ya Ubungo yenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni 1.58 na kueelekeza mitambo hiyo kutumika vyema kutatua changamoto za ubovu wa barabara kwa wananchi
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa mitambo hiyo Profesa Kabudi amesema uzinduzi huo wa mitambo ya miundombinu ni hatua kubwa ya maendeleo kwani moja ya changamoto kubwa kwa wananchi ni ubovu wa barabara hasa nyakati za mvua hivyo mitambo hiyo ni suluhisho la changamoto hiyo ambapo ameagiza mitambo hiyo kutunzwa ili ihudumu kwa muda mrefu
Aidha Kabudi ameongeza kuwa ni muhimu kwa mradi huo kufanywa kuwa endelevu na wenye tija stahiki ili Halmashauri zingine zijifunze kupitia Wilaya ya Ubungo namna bora ya kumaliza changamoto za barabara kwa kuwa na mitambo yao ya ujenzi pia amewataka wananchi kushiriki kuilinda mitambo hiyo dhidi ya hujuma
Kwa upande wa Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam Mhe Albert Chalamila amesema wilaya ya Ubungo imeanza kuwekeza kwenye miradi mikubwa inayoakisi maisha halisi ya wananchi hivyo mitambo hiyo inakwenda kuwa suluhisho la changamoto za maisha ya wananchi hasa kwenye suala la miundombinu ya barabara
Naye Mkuu wa wilaya ya Ubungo wakili Albert Msando amesema uamuzi wa ununuzi wa mitambo hiyo ni kuimarisha zoezi la ukarabati wa barabara wilayani humo ili kumaliza changamoto ya miundombinu ya barabara kwa wananchi
Vilevile katika ziara hiyo pamoja na uzinduzi wa mradi wa mitambo ya ujenzi wa miundombinu pia amekagua ujenzi wa jengo la DMDP wilaya Ubungo pamoja na barabara ya kizota iliopo changanyikeni wilayani Kinondoni ikiwa ni sehemu ya maelekezo ya Rais Dokta Samia Suluhu Hassan ambaye ametaka mawaziri kutembea mikoa yote kukagua miradi ya maendeleo kwa masilahi mapana ya wananchi.













Hakuna maoni: