TANESCO YATAJA MRADI WA DOLA MILIONI 282 KUIMARISHA UMEME ZANZIBAR, KUKUZA NISHATI SAFI
Na Mwandishi Wetu.
Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), Lazaro Twange, amezungumza na Rais wa Zanzibar, Dkt. Hussein Ali Mwinyi, kuhusu utekelezaji wa mradi wa dola za Marekani milioni 282 unaolenga kuimarisha upatikanaji wa umeme Zanzibar pamoja na kukuza matumizi ya nishati safi ya kupikia kupitia umeme.
Twange alitoa maelezo hayo Julai 13, 2026, katika Maonesho ya 50 ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam (Sabasaba), ambapo alimweleza Rais Mwinyi hatua mbalimbali zinazotekelezwa na TANESCO katika kuimarisha sekta ya nishati.
Baadaye akizungumza na waandishi wa habari, Twange alisema zaidi ya dola za Marekani milioni sita za mradi huo zimetengwa mahsusi kwa ajili ya kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia, huku TANESCO ikishirikiana na Shirika la Umeme Zanzibar (ZECO) kuhakikisha wananchi wa Zanzibar na Tanzania Bara wananufaika na huduma hiyo.
Alisema miongoni mwa shughuli muhimu za mradi huo ni ujenzi wa njia mpya za kusafirisha umeme kutoka Tanzania Bara kwenda Zanzibar kupitia nyaya zitakazopita chini ya bahari. Njia hizo zitahusisha Dar es Salaam–Unguja, Tanga–Pemba na Kisiju–Mafia.
Kwa mujibu wa Twange, mhandisi mshauri wa mradi anatarajiwa kupatikana mwezi Agosti mwaka huu, huku mkandarasi akitarajiwa kuanza kazi Januari mwakani. Utekelezaji wa mradi huo unatarajiwa kuchukua kati ya miezi 20 hadi 22.
Alisema kukamilika kwa mradi huo kutaongeza uwezo wa kusambaza umeme Zanzibar, ambako mahitaji yanaendelea kuongezeka kutokana na ukuaji wa sekta za utalii, viwanda na huduma za kijamii.
Katika hatua nyingine, Twange alisema TANESCO inaendelea kutekeleza mpango wa Bill Financing, unaowezesha wananchi kupata majiko ya umeme kwa mkopo na kulipa gharama zake taratibu kupitia ununuzi wa umeme.
Alieleza kuwa zaidi ya asilimia 90 ya wanufaika wa mpango huo wameendelea kurejesha mikopo yao kwa ufanisi, hatua iliyowezesha TANESCO kushirikiana na sekta binafsi kusambaza majiko ya umeme kwa wananchi wengi zaidi.
Aidha, alisema shirika linaendelea kuwekeza katika teknolojia za kisasa, ikiwemo mfumo wa Smart House utakaomwezesha mteja kufuatilia matumizi ya umeme kupitia simu ya mkononi. Pia, TANESCO inaendelea na kampeni ya "Pika na Uendeshe kwa Umeme" inayolenga kuhamasisha matumizi ya umeme katika shughuli za kupikia na matumizi mengine ya kila siku, ikiwa ni sehemu ya juhudi za Serikali kukuza matumizi ya nishati safi nchini.

Hakuna maoni: