TANZANIA MBIONI KUANZA UCHIMBAJI WA CHUMA KWA MARA YA KWANZA: MITAMBO YA KISASA YAWASILI MAGANGA MATITU
NJOMBE.
Tanzania ipo katika hatua za mwisho za kuandika historia mpya katika sekta ya madini na viwanda baada ya mitambo mikubwa ya kisasa ya uchimbaji wa madini ya chuma kuwasili Makambako, mkoani Njombe, ikiwa njiani kuelekea eneo la Mradi wa Maganga Matitu uliopo Wilaya ya Ludewa.
Kuwasili kwa mitambo hiyo kunaashiria kuanza rasmi kwa utekelezaji wa mradi huo wa kimkakati unaotekelezwa kwa ushirikiano kati ya Shirika la Taifa la Maendeleo (NDC) na kampuni ya Fujian Hexingwang Industry Tanzania Limited (Fujian).
Mradi wa Maganga Matitu utahusisha uchimbaji wa madini ya chuma katika eneo lenye ukubwa wa takribani kilomita za mraba 19 pamoja na ujenzi wa kiwanda cha kuchakata chuma ghafi. Mradi huo unahusisha vijiji vya Mundindi, Ilininda, Shauri Moyo na Amani vilivyopo Wilaya ya Ludewa, na unatarajiwa kuwa miongoni mwa miradi mikubwa ya kimkakati itakayochochea maendeleo ya sekta ya madini, viwanda na uchumi wa Taifa.
Akizungumza baada ya kuwasili kwa mitambo hiyo, Mkurugenzi Mtendaji wa NDC, Dkt. Nicolaus Shombe, alisema hatua hiyo ni ushahidi wa dhamira ya Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kuhakikisha Tanzania inaanza kuchimba na kunufaika kikamilifu na rasilimali zake za madini ya chuma.
"Kuwasili kwa mitambo hii ni hatua kubwa kuelekea utekelezaji wa mradi ambao utabadilisha historia ya sekta ya madini ya chuma nchini. Zaidi ya dola za Marekani milioni 70 zinawekezwa katika mradi huu ambao utafungua ukurasa mpya wa maendeleo ya uchumi wa Mkoa wa Njombe na Tanzania kwa ujumla," alisema Dkt. Shombe.
Alisema kwa sasa Tanzania hutumia zaidi ya dola za Marekani bilioni 1.22, sawa na takribani Sh trilioni 3.2, kuagiza bidhaa za chuma kutoka nje ya nchi, hali inayofanya sekta hiyo kushika nafasi ya pili kwa matumizi makubwa ya fedha za kigeni baada ya mafuta.
Dkt. Shombe aliongeza kuwa NDC itaendelea kushirikiana kwa karibu na kampuni ya Fujian kuhakikisha ndoto ya muda mrefu ya Tanzania kuwa na mradi mkubwa wa uchimbaji wa madini ya chuma inakuwa uhalisia.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kijiji cha Mundindi, Steven Sapi Mlewa, alisema wananchi wameupokea mradi huo kwa matumaini makubwa kutokana na fursa za ajira, biashara na maendeleo zitakazotokana nao.
"Kwa miaka mingi tulikuwa tunasikia kuhusu Mradi wa Maganga Matitu, lakini leo tunaona utekelezaji wake kwa vitendo. Kuwasili kwa mitambo kunatupa matumaini mapya ya ajira kwa vijana, kuboresha huduma za jamii na kukuza uchumi wa wananchi wetu," alisema.
Naye Meneja wa Mradi, Mhandisi Wallu Kapaya, alisema mradi huo unatarajiwa kuwa kichocheo kikubwa cha ukuaji wa uchumi wa Taifa kupitia uzalishaji wa malighafi muhimu kwa viwanda, ongezeko la mapato ya Serikali na kuimarisha sekta nyingine zinazotegemea shughuli za uchimbaji.
Alisema mradi huo unatarajiwa kuzalisha zaidi ya ajira 1,000 za moja kwa moja na zisizo za moja kwa moja, huku ukichochea maendeleo ya miundombinu ikiwemo barabara, huduma za jamii, biashara na uwekezaji katika maeneo yanayouzunguka.
Afisa Mtendaji wa Kijiji cha Mundindi, Adrat Msigwa, alisema Serikali imeendelea kutoa elimu kwa wananchi kuhusu umuhimu wa mradi huo na namna ya kutumia fursa zitakazojitokeza.
"Tunaendelea kuwahamasisha wananchi kujiandaa kunufaika na ajira, biashara ndogo ndogo pamoja na utoaji wa huduma mbalimbali zitakazotokana na mradi huu," alisema.
Baadhi ya wananchi wa Kijiji cha Mundindi walisema utekelezaji wa mradi huo unaashiria mwanzo wa zama mpya za maendeleo katika eneo hilo.
Mkazi wa kijiji hicho, Jonisia Mlowe, alisema vijana wengi wamekuwa wakihama kwenda mikoa mingine kutafuta ajira, lakini sasa wana matumaini ya kupata kazi karibu na makazi yao.
"Tunafurahi kuona mradi umeanza kwa vitendo. Tunaamini vijana wengi sasa watapata ajira hapa nyumbani badala ya kuhangaika kwenda mbali kutafuta maisha," alisema.
Naye mfanyabiashara Moses Mwakalinga alisema kuongezeka kwa shughuli za mradi kutafungua fursa nyingi za biashara, huku akisisitiza umuhimu wa vijana wa maeneo yanayouzunguka mradi kupewa kipaumbele katika ajira na mafunzo ya ujuzi.
"Kadri shughuli za mradi zitakavyoongezeka, ndivyo mahitaji ya chakula, malazi, usafiri na huduma nyingine yatakavyoongezeka, jambo ambalo litaongeza kipato cha wananchi," alisema.
Wakati huo huo, maandalizi mengine ya utekelezaji wa mradi yanaendelea ambapo TANESCO tayari imeanza kusambaza umeme kwa kujenga miundombinu ya nguzo kuelekea eneo litakapojengwa kiwanda cha uchakataji wa madini ya chuma.
Ujenzi wa mradi huo unatarajiwa kukamilika ndani ya miaka miwili, hatua itakayowezesha Tanzania kuanza kunufaika kwa kiwango kikubwa na rasilimali zake za madini ya chuma.
Mradi huo unatekelezwa na NDC kama mwekezaji wa kimkakati kwa niaba ya Serikali kwa kushirikiana na kampuni ya Fujian. Uwekezaji huo unatajwa kuwa na mchango mkubwa katika utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 kupitia uendelezaji wa rasilimali za kimkakati zenye manufaa makubwa kwa uchumi wa Taifa.
Kwa mujibu wa taarifa za uhakiki wa mashapo, Mradi wa Maganga Matitu una akiba ya tani milioni 101 za madini ya chuma, na hivyo kuwa mradi wa pili kwa ukubwa nchini baada ya Mradi wa Liganga wenye zaidi ya tani milioni 126.
Kuanza kwa utekelezaji wa Mradi wa Maganga Matitu kunatajwa kuwa hatua muhimu katika safari ya Tanzania kuelekea uchumi wa viwanda kwa kuongeza thamani ya rasilimali za ndani, kupunguza utegemezi wa uagizaji wa bidhaa za chuma kutoka nje ya nchi, kuongeza mapato ya Serikali na kufungua maelfu ya fursa za ajira na biashara kwa wananchi.


Hakuna maoni: