TTCL YAONESHA MABADILIKO YA KIDIJITALI SABA SABA, YALETA HUDUMA MPYA ZA INTANETI NA CLOUD

 TTCL YAONESHA MABADILIKO YA KIDIJITALI SABA SABA, YALETA HUDUMA MPYA ZA INTANETI NA CLOUD

Shirika la Mawasiliano Tanzania TTCL Corporation limeendelea kuonesha mageuzi makubwa ya kiteknolojia kupitia huduma mbalimbali za kidijitali, ikiwemo intaneti ya kasi ya juu, huduma za “smart home”, pamoja na miundombinu ya uhifadhi na usindikaji wa data (cloud services) katika Maonesho ya Sabasaba jijini Dar es Salaam.

Akizungumza katika banda la TTCL, katika maonyesho ya kimataifa yabiashara ya sabasaba, Mkurugenzi Mkuu wa shirika hilo Moremi Marwa amesema kuwa huduma wanazotoa zinategemea kwa kiasi kikubwa Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano, ambao umeendelea kuwa mhimili muhimu wa kuunganisha mifumo ya serikali na kukuza uchumi wa kidijitali nchini.

Ameeleza kuwa TTCL imezindua huduma za intaneti ya kasi ya juu na gharama nafuu, akisisitiza kuwa kampuni hiyo ina uwezo wa kutoa huduma zenye kasi kubwa zaidi ikilinganishwa na baadhi ya watoa huduma wengine sokoni.

Katika maonesho hayo, TTCL pia imeonesha Kituo cha Uzoefu wa Teknolojia (FTTX Experience Centre), ambacho kinaonesha matumizi ya intaneti katika kuendesha maisha ya kisasa, ikiwemo nyumba mahiri (smart home). Kupitia teknolojia hiyo, vifaa vya nyumbani kama taa, televisheni, friji, jiko na mifumo ya ulinzi vinaweza kuunganishwa na kudhibitiwa kwa njia ya mtandao.

Aidha, shirika hilo limeonesha huduma za kituo chake cha data kinachowezesha huduma za cloud, ambapo taasisi na wateja binafsi wenye uhitaji wa kuhifadhi data bila kuwekeza miundombinu mikubwa wanaweza kununua nafasi kwenye mfumo huo.

Mkurugenzi huyo amesisitiza kuwa huduma hizi zote zinaendana na matumizi ya Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano, unaowezesha upatikanaji wa mtandao wa fiber unaochochea ufanisi wa huduma za kidijitali na ukuaji wa uchumi wa kidijitali nchini.

Kuhusu matokeo ya kifedha, amesema TTCL iliendelea kuimarika na kufanikiwa kupata faida ya takribani shilingi bilioni 23 katika mwaka wa fedha 2024/25. Ameongeza kuwa kwa mwaka wa 2025/26, matokeo rasmi yatatangazwa baada ya ukaguzi kukamilika, lakini dalili zinaonesha ongezeko la mapato na faida.

Amesema mabadiliko yaliyofanyika ndani ya shirika hilo, kufuatia maelekezo ya Serikali, yameiwezesha TTCL kujiendesha kibiashara zaidi huku ikiendelea kuboresha huduma kwa wateja na kuchangia ukuaji wa uchumi wa kidijitali nchini.

“Ninaamini kipindi cha hasara kimepita. Sasa tunaelekea kwenye ukuaji endelevu wa mapato na faida,” amesema.

Shirika hilo limeendelea kusisitiza dhamira yake ya kuimarisha huduma za mawasiliano na kuifanya Tanzania kuwa kitovu cha teknolojia za kidijitali kupitia miundombinu ya kisasa ya mtandao.

Hakuna maoni:

Inaendeshwa na Blogger.