VITUMBUA FESTIVAL KUFANYIKA DAR, KUINUA HADHI YA WACHOMA VITUMBUA NA KUHAMASISHA NISHATI SAFI

DAR ES SALAAM.

Umoja wa Mama na Baba Lishe Tanzania (UMALITA) umetangaza kuanzishwa rasmi kwa tamasha la kwanza la Vitumbua Festival, litakalofanyika Julai 30, 2026, katika Viwanja vya Mnazi Mmoja jijini Dar es Salaam kuanzia saa 12:00 asubuhi.

Tamasha hilo linalenga kuinua hadhi ya wachoma vitumbua, kuongeza thamani ya kiuchumi ya biashara hiyo, pamoja na kutambua mchango wao katika kukuza uchumi na kuunda fursa za ajira nchini.

Akizungumza kuhusu maandalizi ya tamasha hilo, Mwenyekiti wa UMALITA Taifa, Avijawa Omary (Afidhal Omari Tebani), amesema mashindano ya kuchoma vitumbua yatawakutanisha washiriki kutoka wilaya zote za Mkoa wa Dar es Salaam, huku washindi wakitarajiwa kujinyakulia zawadi mbalimbali.

Amesema mshindi wa kwanza atazawadiwa fedha taslimu, kiwanja pamoja na eneo maalumu la kuendeshea biashara ya vitumbua, huku washindi wa pili na wa tatu wakipatiwa fedha taslimu, vifaa vya biashara na zawadi nyingine mbalimbali.

Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa UMALITA, Johajulieth Madata, amesema tamasha hilo pia litatumika kuunga mkono kampeni ya Serikali ya kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia.

Ameeleza kuwa wachoma vitumbua watapatiwa elimu kuhusu matumizi ya gesi ya kupikia (LPG) badala ya kuni na mkaa, hatua ambayo itasaidia kuboresha afya zao, kulinda mazingira, kuongeza usafi na ufanisi katika maandalizi ya chakula hicho cha asili.

Baadhi ya wajasiriamali wanaojishughulisha na biashara ya vitumbua wameeleza matumaini yao kuwa tamasha hilo litachangia kuboresha mazingira ya biashara zao, kuongeza kipato na kuwapa fursa ya kutambulika zaidi katika jamii.

Hakuna maoni:

Inaendeshwa na Blogger.