Naibu Waziri wa Nishati amesema vyombo vya habari na maafisa mawasiliano Serikalini ni washirika muhimu wa maendeleo ya Taifa kutokana na nafasi yao ya kufikisha taarifa sahihi kwa wananchi na kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia kupitia habari, vipindi vya redio na televisheni pamoja na majukwaa ya kidijitali.
Hayo ameyabainisha leo Julai 15, 2026 wakati akifungua Warsha ya Kuwajengea Uwezo Waandishi wa Habari na Maafisa Mawasiliano Serikalini kutoka katika Wizara na Taasisi kuhusu Uandishi na Uhamasishaji wa Masuala ya Nishati Safi ya Kupikia, inayofanyika katika ukumbi wa Morena hoteli mkoani Morogoro.
Amesema vyombo vya habari si wasambazaji wa taarifa pekee bali ni washirika muhimu wa maendeleo ya Taifa kwa kutoa taarifa sahihi huku akibainisha kuwa kupitia habari, vipindi vya redio na televisheni, makala pamoja na maudhui ya kidijitali, wanahabari wana nafasi kubwa ya kujenga uelewa wa wananchi, kuondoa dhana potofu na kuhamasisha mabadiliko chanya ya tabia kuhusu matumizi ya nishati safi ya kupikia kwani katika zama za mawasiliano ya kidijitali, taarifa moja sahihi inaweza kuwafikia mamilioni ya wananchi ndani ya muda mfupi na kuleta mabadiliko makubwa katika jamii.
Amefafanua kuwa, taarifa zisizo sahihi zinaweza kusababisha upotoshaji na kuchelewesha utekelezaji wa ajenda muhimu za maendeleo akimnukuu Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, wakati wa ufunguzi wa Mkutano Mkuu wa Mwaka wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS) uliofanyika jijini Arusha, amesema watu wanaweza kushiriki kubomoa Tanzania, lakini hawawezi kusaidia kuijenga hivyo amesisitiza kuwa wanahabari wana wajibu wa kutumia kalamu na keybord zao kuandika habari zenye ukweli, zenye kujenga matumaini na kuunga mkono juhudi za maendeleo ya Taifa badala ya taarifa zinazoweza kupotosha wananchi.
Aidha Mhe. Salome ameeleza kuwa, matarajio ya Serikali ni kuwa mafunzo hayo yatawaongezea washiriki maarifa na ujuzi wa kuandaa habari zenye usahihi, ushahidi na weledi wa hali ya juu, pamoja na kuandaa maudhui yanayoonesha mafanikio ya utekelezaji wa miradi ya nishati safi ya kupikia, ubunifu wa sekta binafsi na fursa zilizopo katika mnyororo wa thamani wa sekta hiyo.
Ameongeza kuwa warsha hiyo itawajengea uwezo washiriki kuhusu sera, mikakati na mwelekeo wa Serikali katika sekta ya nishati safi ya kupikia, matumizi sahihi ya takwimu pamoja na namna bora ya kuripoti kuhusu teknolojia mbalimbali zinazopatikana nchini ili kuandaa taarifa zenye ubora na zinazojenga uelewa wa wananchi.
Aidha, amewataka washiriki kutumia kikamilifu fursa ya mafunzo hayo kujenga ushirikiano kati ya Wizara ya Nishati, Idara ya Habari MAELEZO, washirika wa maendeleo, sekta binafsi na vyombo vya habari, akisisitiza kuwa mawasiliano sahihi ni nguzo muhimu ya kufanikisha ajenda ya nishati safi ya kupikia na kufikia lengo la asilimia 80 ya matumizi ifikapo mwaka 2034.




Hakuna maoni: