Wanahabari wametakiwa kuwa mstari wa mbele katika kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia ikiwa ni ajenda ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ili kuchangia kufikiwa kwa lengo la Taifa la asilimia 80 ya matumizi ya nishati safi ya kupikia ifikapo mwaka 2034.
Wito huo umetolewa Julai 16, 2026 na Mkurugenzi Msaidizi kutoka Idara ya Habari Maelezo , Bw. Rodney Mbuya, wakati akifunga Warsha ya Kuwajengea Uwezo Waandishi wa Habari pamoja na Maafisa Mawasiliano wa Serikali kuhusu Uandishi na Uhamasishaji wa Masuala ya Nishati Safi ya Kupikia mkoani Morogoro.
Bw. Mbuya amesema Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, imeipa kipaumbele ajenda ya nishati safi ya kupikia kupitia Mkakati wa Taifa wa Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia wa miaka 10 (2024–2034).
Amesema pamoja na mafanikio yaliyofikiwa ambapo matumizi ya nishati safi ya kupikia nchini yamefikia asilimia 28.6 ya kaya, bado kuna umuhimu wa kuongeza kasi ya utoaji wa elimu kwa umma kupitia vyombo vya habari ili kuhakikisha lengo la Taifa linafikiwa kwa wakati. Aidha, amesisitiza kuwa vyombo vya habari vya kitaifa na vya mikoani vina mchango mkubwa katika kuhamasisha jamii kubadili tabia na kukumbatia matumizi ya nishati safi ya kupikia.
Aidha ameipongeza Wizara ya Nishati, Shirika la Umoja wa Mataifa la Mfuko wa Maendeleo ya Mitaji (UNCDF) kupitia Mradi wa CookFund unaofadhiliwa na Umoja wa Ulaya pamoja na wadau wote wa nishati safi ya kupikia kwa kuandaa mafunzo hayo, akieleza kuwa yataongeza uwezo wa Waandishi wa Habari na Maafisa Mawasiliano wa Serikali katika kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia nchini.
Vilevile, ameitaka Wizara ya Nishati kuendelea kuimarisha utekelezaji wa Mkakati wa Taifa kwa kuandaa mpango mahsusi wa utekelezaji, kuwashirikisha viongozi wa ngazi za msingi katika utoaji wa elimu kwa wananchi na kuhakikisha maazimio yaliyotolewa na washiriki wa warsha yanafanyiwa kazi kwa lengo la kuboresha utekelezaji wa ajenda ya nishati safi ya kupikia nchini.



Hakuna maoni: