WANANCHI WA WILAYA YA MBOGWE WAIPONGEZA SERIKALI KWA UTATUZI WA KERO YA MAJI











Mbogwe – Geita

Serikali imejipanga kuachana na mipango inayobaki kwenye makaratasi na kuelekeza nguvu katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo kwa vitendo, kwa mujibu wa maelekezo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Kauli hiyo imetolewa leo Julai 23, 2026 na Waziri wa Madini, Mhe. Anthony Mavunde, wakati akizungumza na wananchi katika mkutano wa hadhara uliofanyika Kijiji cha Lugunga, Wilaya ya Mbogwe mkoani Geita, ikiwa ni sehemu ya ziara yake ya kukagua na kuzindua miradi ya maendeleo.

Akiendeleza ziara yake, Waziri Mavunde amezindua mradi wa maji safi na salama wenye thamani ya zaidi ya Shilingi bilioni 2.5 katika Kijiji cha Ushirika. Mradi huo una uwezo wa kuhifadhi lita 150,000 za maji na unatarajiwa kuhudumia zaidi ya wananchi 21,000 kutoka vijiji sita vya Wilaya ya Mbogwe.

Akizungumza katika mkutano huo, Waziri Mavunde amesema Serikali imefanikiwa kuunganisha miundombinu ya msingi kati ya mikoa na wilaya, na sasa inaelekeza nguvu katika kuboresha mtandao wa barabara za ndani ili kuchochea shughuli za kiuchumi na kurahisisha upatikanaji wa huduma za kijamii.

Amesema kwa Mkoa wa Geita, Serikali imepanga kuleta fedha kwa ajili ya ujenzi wa kilomita 102 za barabara katika maeneo mbalimbali ya vijiji.

"Mimi kama Mlezi wa Maendeleo wa Mkoa wa Geita nawaahidi wananchi wa Mbogwe kuwa nitaendelea kushirikiana na Serikali kuhakikisha tunaleta taa za barabarani ili kuongeza usalama na kuboresha mazingira ya biashara na huduma," amesema Waziri Mavunde.

Katika mkutano huo, Waziri Mavunde pia ametoa elimu kuhusu Sheria ya Madini, akieleza kuwa kila Mtanzania ana haki ya kumiliki leseni ya madini kwa kufuata taratibu zilizowekwa na sheria. Amesisitiza kuwa mwenye leseni haruhusiwi kuanza shughuli za uchimbaji katika eneo la mtu mwingine bila kufikia makubaliano na mmiliki wa ardhi husika.

Akijibu maswali ya wananchi, Waziri Mavunde amesema Serikali inaendelea na mpango wa kusambaza nishati ya umeme katika maeneo ya uchimbaji madini pamoja na maeneo mengine yenye shughuli za uzalishaji ili kuongeza tija ya kiuchumi na kuvutia uwekezaji.

Katika hatua nyingine, Waziri Mavunde amezindua bweni la wanafunzi katika Shule ya Sekondari Nyakasaluma, mradi unaotarajiwa kuboresha mazingira ya kujifunzia na kuongeza ufaulu wa wanafunzi wa shule hiyo.

Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Geita, Martin Shigella, amempongeza Waziri Mavunde kwa kuendelea kusimamia kwa karibu utekelezaji wa miradi ya maendeleo na kutatua changamoto za sekta ya madini mkoani humo tangu alipoteuliwa kuwa Mlezi wa Maendeleo wa Mkoa wa Geita.

Aidha, Mkuu huyo wa Mkoa amemuomba Waziri Mavunde kuendelea kuisadia Serikali katika kuharakisha ujenzi wa barabara za Wilaya ya Mbogwe pamoja na kuhamasisha utekelezaji wa mpango wa Bima ya Afya kwa Wote.

Naye Mbunge wa Mbogwe, Mhe. Alon Fagason, alimpongeza Waziri Mavunde kwa kuendelea kuleta na kuzindua miradi ya maendeleo wilayani humo, akisema miradi hiyo itaboresha maisha ya wananchi wa Mbogwe na Mkoa wa Geita kwa ujumla pamoja na kuchochea maendeleo ya kiuchumi katika maeneo ya jirani.

Hakuna maoni:

Inaendeshwa na Blogger.