WAZIRI MAVUNDE AELEKEZA USIMAMIZI THABITI WA SHERIA ILI ASILIMIA 90 YA BIDHAA NA HUDUMA MIGODINI KUFANYWA NA WATANZANIA
MWANZA
Waziri wa Madini, Mheshimiwa Anthony P. Mavunde, ameelekeza usimamizi madhubuti wa Sheria ya Madini na kanuni zake ili kuhakikisha asilimia 90 ya bidhaa na huduma zinazotumika katika migodi nchini zinatolewa na Watanzania, hatua inayolenga kuongeza ushiriki wa wananchi na kukuza uchumi wa nchi.
Waziri Mavunde ametoa maelekezo hayo mapema leo Julai 22, 2026, wakati akizindua Jukwaa la Tano la Utekelezaji wa Ushirikishwaji wa Watanzania katika Sekta ya Madini, lililofanyika Mwanza na kuwakutanisha wadau mbalimbali wa sekta hiyo, wakiwemo kampuni za uchimbaji wa madini, watoa huduma migodini, wafanyabiashara wa madini, wawekezaji, taasisi za umma na binafsi pamoja na vyama vya wachimbaji wa madini nchini.
Amesema utekelezaji madhubuti wa Sheria ya Madini na kanuni zake utasaidia kuongeza ushiriki wa Watanzania katika uzalishaji wa bidhaa na utoaji wa huduma migodini, sambamba na kuhakikisha fursa zinazotokana na ukuaji wa Sekta ya Madini zinawanufaisha wananchi na biashara za ndani.
“Serikali inatarajia kuona asilimia 90 ya bidhaa na huduma zinazotumika katika migodi zikizalishwa na kutolewa na Watanzania. Hili linahitaji usimamizi madhubuti wa sheria, pamoja na Watanzania kujiandaa kutumia fursa zinazopatikana katika Sekta ya Madini,” amesema.
Waziri Mavunde amewataka watoa huduma katika migodi nchini kuunganisha nguvu na kufanya kazi kwa pamoja ili kuchangamkia fursa zinazoongezeka katika sekta hiyo, hususan katika uzalishaji wa bidhaa na utoaji wa huduma bora zinazokidhi viwango vinavyohitajika.
Amesema ongezeko la uwekezaji katika Sekta ya Madini na matarajio ya kuanzishwa kwa migodi mipya linatarajiwa kufungua fursa zaidi kwa Watanzania, hivyo watoa huduma wanapaswa kujiandaa kwa kuwekeza katika uzalishaji wa ndani, kuongeza ubora wa bidhaa na huduma na kujenga uwezo wa kushindana katika soko.
“Watoa huduma wanapaswa kuungana na kufanya kazi kwa pamoja ili kutoa huduma zenye ubora wa hali ya juu na kuchangamkia fursa zinazopatikana katika Sekta ya Madini. Hii itawasaidia kukua kibiashara na pia kuchangia katika kukuza uchumi wa nchi,” amesema Waziri Mavunde.
Wakati huo huo, Waziri Mavunde ametoa angalizo kwa wawekezaji katika Sekta ya Madini kuhakikisha wanazingatia na kutii sheria na kanuni za nchi zinazosimamia sekta hiyo.
“Serikali imeboresha mazingira ya uwekezaji kwa kuweka sheria na kanuni ambazo mnapaswa kuzifuata ili uwekezaji wenu uwe na tija nchini,” amesisitiza.
Akielezea mafanikio yaliyopatikana tangu kufanyika kwa maboresho ya Sheria ya Madini na kanuni zake, Waziri Mavunde amesema Serikali imeendelea kushuhudia ongezeko la ushiriki wa Watanzania katika utoaji wa huduma na usambazaji wa bidhaa kwenye migodi.
Amesema ununuzi wa bidhaa na huduma katika Sekta ya Madini umefikia Shilingi trilioni 5.1 kwa mwaka, hali inayoonesha ukubwa wa fursa zilizopo kwa wazalishaji na watoa huduma wa ndani.
Aidha, amesema Sekta ya Madini imezalisha ajira rasmi 20,421, ambapo ajira 16,695 zinashikiliwa na Watanzania.
“Mpaka sasa tumeshuhudia watendaji wakuu na mameneja wa migodi wakiwa Watanzania. Haya ni mafanikio makubwa tofauti na zamani, ambapo nafasi nyingi za uongozi katika migodi ya madini zilishikiliwa na raia wa kigeni,” amesisitiza.
Waziri Mavunde amesema mafanikio mengine ni kuanzishwa kwa masoko ya madini 44 na vituo vya ununuzi wa madini 117, hatua ambayo imechangia kuongeza ukusanyaji wa maduhuli yatokanayo na Sekta ya Madini kutoka Shilingi bilioni 161 katika mwaka wa fedha 2015/2016 hadi Shilingi trilioni 1.393 katika mwaka wa fedha 2025/2026.
Aidha, amesema utekelezaji wa maelekezo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, ya kuanzisha hifadhi ya dhahabu katika Benki Kuu ya Tanzania, ulioanza rasmi Oktoba 1, 2024, umeiwezesha Tanzania kuwa na hifadhi ya dhahabu yenye uzito wa tani 28 na kuiweka nchi miongoni mwa mataifa matano barani Afrika yenye hifadhi kubwa ya dhahabu.
Amesema mchango wa Sekta ya Madini katika Pato la Taifa umeendelea kuongezeka na kufikia asilimia 10.1, hatua inayoonesha umuhimu wa sekta hiyo katika kukuza uchumi wa nchi.
Waziri Mavunde amempongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuipa kipaumbele Sekta ya Madini na kuendelea kuweka mazingira wezeshi ya uwekezaji na ushiriki wa Watanzania katika sekta hiyo.
Pia amewapongeza Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini kwa usimamizi madhubuti wa Sekta ya Madini, pamoja na Menejimenti ya Wizara ya Madini na Tume ya Madini kwa uchapakazi na ubunifu unaochangia kuiwezesha sekta hiyo kuendelea kufanya vizuri.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Mhandisi Yahya Samamba, amesema Serikali imeendelea kuweka mazingira mazuri ya uwekezaji katika Sekta ya Madini ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050.
Amewataka watoa huduma katika migodi kutoa huduma bora kwa kuzingatia weledi, uadilifu na viwango vinavyokubalika, akisisitiza kuwa Wizara itaendelea kutekeleza maelekezo ya Serikali na kufanya kazi kwa karibu zaidi na wadau wa Sekta ya Madini.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Ilemela, Amir Mkalipa, akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Said Mtanda, ameipongeza Wizara ya Madini kwa juhudi zake za kuendelea kuvutia uwekezaji katika Mkoa wa Mwanza.
Amesema uwekezaji huo umechangia kuanzishwa kwa Mgodi wa Dhahabu wa Sotta Mining, ambao unatarajiwa kutoa ajira 1,500 utakapoanza uzalishaji.
Naye Mwenyekiti wa Tume ya Madini, Dkt. Janet R. Lekashingo, amesema Jukwaa la Utekelezaji wa Ushirikishwaji wa Watanzania katika Sekta ya Madini limekuwa na manufaa makubwa katika kuchochea ushiriki wa Watanzania katika sekta hiyo.
Amesema mafanikio hayo yanaonekana kupitia ongezeko la uwasilishaji wa mipango ya ushirikishwaji wa Watanzania katika Sekta ya Madini, kutoka mipango 51 mwaka 2018 hadi kufikia mipango 1,312 mwaka 2025.









Hakuna maoni: