Na Mwandishi Wetu,
Zanzibar.
ZANZIBAR. Mfanyabiashara na mfugaji wa nyuki, Salim Faraj Abri (ASAS), amevutiwa na mbinu za kisasa za ufugaji nyuki alizopewa na wataalamu wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS), akisema elimu hiyo itamsaidia kuongeza uzalishaji wa asali katika shughuli zake za ufugaji wilayani Mufindi, Iringa.
Abri, ambaye anamiliki Kampuni ya Asas Diaries, alisema amekuwa akifuga nyuki Mufindi na tayari ana mizinga iliyowekwa kwenye miti, lakini elimu aliyopata kuhusu matumizi ya vifaa na mbinu bora za kisasa imemfungulia fursa mpya za kuboresha ufugaji wake.
“Mimi ni mfugaji mzuri wa nyuki. Angalia picha hizi, nina mizinga ambayo nimeitundika kwenye miti na shughuli zangu nazifanyia Wilaya ya Mufindi,” alisema Abri.
Alisema elimu hiyo, ambayo ameipata katika banda la Wizara ya Maliasili na Utalii kwenye Tamasha la Kizimkazi, itakuwa na mchango katika kuongeza tija na uzalishaji wa mazao yatokanayo na ufugaji wa nyuki.
Abri alitoa kauli hiyo leo, Agosti 12, 2026, katika Ufunguzi wa Tamasha la Kizimkazi unaofanyika katika Uwanja wa Kizimkazi, Zanzibar, lenye kaulimbiu “Kizimkazi Kumenoga, Shangwe na Fursa.”
Kwa upande wake, Mhifadhi Mwandamizi Ufugaji Nyuki kutoka TFS, SCO. Said Aboubakar, alisema matumizi ya mbinu za kisasa katika ufugaji nyuki yanaweza kuongeza uzalishaji wa asali huku yakisaidia kulinda rasilimali za misitu, hivyo kuwataka wafugaji kutumia njia zinazozingatia usalama na mazingira.
“Sasa hivi tunafuga kisasa. Sio lazima mizinga itundikwe kwenye miti kama tulivyozoea; sasa tunaweka kwenye vichanja au kejeli na tunatumia mavazi kinga ya nyuki,” alisema SCO. Said.
TFS imeendelea kutoa elimu katika banda lake kwenye Tamasha la Kizimkazi kuhusu ufugaji nyuki wa kisasa, uhifadhi wa rasilimali za misitu na utalii wa ikolojia, ikiwaalika wananchi na wadau kutembelea banda hilo na kupata elimu na fursa zinazohusiana na sekta hizo.



Hakuna maoni: