Na Mwandishi Wetu.
MKUU wa Chuo cha Bahari Dar es Salaam (DMI), Dk. Tumaini Gurumo, amesema Tanzania inahitaji kuongeza idadi ya wataalamu wa usafirishaji na usimamizi wa mnyororo wa usambazaji wa bidhaa ili kuongeza tija, ushindani wa bidhaa za ndani na kufikia malengo yaliyowekwa katika Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.
Dk. Gurumo amesema hayo leo jijini Dodoma wakati akizungumza na waandishi wa habari katika Maonesho ya 49 ya Nanenane yanayofanyika kwenye Viwanja vya Dk. John Malecela.
Amesema DMI, kinachojulikana kwa kutoa mafunzo yanayohusiana na masuala ya bahari na mabaharia, pia kinatoa mafunzo ya lojistiki pamoja na usimamizi wa mnyororo wa usambazaji wa bidhaa, ambayo ni maeneo muhimu katika kukuza biashara na uchumi wa Tanzania.
Kwa mujibu wa Dk. Gurumo, kilimo na shughuli za bahari haviwezi kutenganishwa kwa kuwa mazao yanayozalishwa nchini yanahitaji mifumo bora ya usafirishaji ili kuwafikia walaji na masoko kwa wakati.
Amesema uwepo wa wataalamu wenye ujuzi katika mnyororo wa usafirishaji ni sehemu muhimu ya maandalizi ya Tanzania kushindana katika masoko ya kimataifa, kwa kuwa ushindani wa kiuchumi hauishii ndani ya mipaka ya nchi.
Akizungumzia matumizi ya akili bandia (AI), Dk. Gurumo amesema DMI imeendelea kuboresha mitaala yake ili kuendana na mabadiliko ya teknolojia, ikiwemo matumizi ya mifumo ya kidijitali na akili bandia katika sekta ya usafirishaji.
Amesema hatua hiyo inalenga kuhakikisha wahitimu wa chuo hicho wanaingia katika soko la ajira wakiwa na ujuzi unaoendana na mahitaji ya sasa ya sekta ya usafirishaji na uchumi kwa ujumla.


Hakuna maoni: