DSE YASAINI HATI YA MAKUBALIANO (MoU) NA TPSF KUWEZESHA BIASHARA KUKUA NA KUPATA MITAJI

Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE) limesaini Hati ya Makubaliano (MoU) na Shirikisho la Sekta Binafsi Tanzania (TPSF ), hatua muhimu inayolenga kuimarisha ukuaji wa biashara za Tanzania kwa kuzijengea uwezo na kuzifungulia fursa za kupata mitaji kupitia soko la mitaji.

Kupitia ushirikiano huu, DSE na TPSF zitatekeleza kwa pamoja DSE Enterprise Acceleration Program (DEAP) pamoja na jukwaa la ENDELEZA, programu zinazolenga kuzisaidia biashara ndogo na za kati (SMEs) kujengea uwezo, kuboresha utayari wa kupata uwekezaji, na kufikia vyanzo mbalimbali vya mitaji.

Wanachama wa TPSF watanufaika na mafunzo ya maendeleo ya biashara, ushauri elekezi (mentorship), utambuzi wa biashara (enterprise profiling), pamoja na fursa za kuunganishwa na wawekezaji, taasisi za fedha na wadau wengine wa maendeleo ya biashara.

Aidha, ushirikiano huu utazijengea biashara uwezo katika maeneo muhimu kama vile utawala bora wa kampuni, uandaaji wa mipango ya biashara, tathmini ya biashara, mbinu za kupata mitaji, na maandalizi ya kushiriki katika masoko ya mitaji ili kukuza biashara zao kwa uendelevu.

Kupitia makubaliano haya, DSE na TPSF zitashirikiana kuhamasisha ushiriki wa wafanyabiashara kutoka maeneo mbalimbali nchini, kukuza utamaduni wa matumizi ya soko la mitaji kama chanzo cha fedha za ukuaji wa biashara, na kuimarisha mazingira ya ujasiriamali yatakayochochea maendeleo jumuishi ya uchumi wa Tanzania.

Ushirikiano huu unaakisi dhamira ya DSE ya kuendelea kuwa daraja linalounganisha biashara zenye fursa za ukuaji na mitaji inayohitajika ili kuzijengea ushindani, kuongeza ajira na kuchangia maendeleo endelevu ya uchumi wa taifa.

Hakuna maoni:

Inaendeshwa na Blogger.