FURSA ZA BIASHARA ZA MABILIONI KATIKA MIGODI ZAWAFUNGUKIA WATANZANIA

Vijana na wanawake wapewa kipaumbele kunufaika na mnyororo wa thamani wa madini

DODOMA.

Serikali kupitia Tume ya Madini imefungua fursa za biashara zenye thamani ya mabilioni ya fedha katika migodi kwa Watanzania, huku vijana na wanawake wakipewa kipaumbele ili kuongeza ushiriki wao katika Sekta ya Madini na kuchochea utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.

Hatua hiyo inalenga kujenga uchumi shindani na jumuishi unaowezesha Watanzania kushiriki kikamilifu katika shughuli za uzalishaji, kuongeza thamani ya rasilimali za madini na kunufaika zaidi na fursa zinazotokana na sekta hiyo.

Akizungumza katika Maonesho ya Nane Nane yanayoendelea katika Viwanja vya Nzuguni, Dodoma, Mjiolojia kutoka Kurugenzi ya Ukaguzi na Biashara ya Madini ya Tume ya Madini, Hassan Mkumba, amesema Tume imeainisha bidhaa na huduma 20 zitakazotolewa mahsusi na Watanzania ili kuongeza ushiriki wao katika shughuli za migodi.

Amezitaja baadhi ya huduma hizo kuwa ni usambazaji wa vilainishi migodini, huduma za usafi, huduma za kisheria zinazohusu sekta ya madini, usambazaji wa kemikali za uchenjuaji, activated carbon, uchimbaji mdogo, uchorongaji, uchambuzi wa maabara za madini, usafirishaji wa madini na huduma za ulinzi migodini.

Mkumba amesema fursa nyingine ni usambazaji wa vifaa vya usalama binafsi (PPE), uhandisi wa mitambo ya madini, matengenezo ya vifaa, usambazaji wa mafuta, upimaji na uchoraji ramani, huduma za ushauri wa kitaalamu pamoja na huduma za upishi na malazi kwa wafanyakazi wa migodini.

Amesema hatua hiyo ni sehemu ya utekelezaji wa sera za Serikali za kuimarisha ushiriki wa wazawa katika mnyororo mzima wa thamani wa madini, kuongeza ajira, kukuza biashara za ndani na kuhakikisha rasilimali za madini zinachangia kwa kiwango kikubwa zaidi katika maendeleo ya uchumi wa Taifa.

Mkumba amewataka vijana, wanawake na wafanyabiashara wa Kitanzania kujitokeza na kutumia fursa hizo kwa kuzingatia viwango na mahitaji ya sekta, akisisitiza kuwa ushiriki wao utachangia kujenga uchumi imara na kufanikisha malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.

Hakuna maoni:

Inaendeshwa na Blogger.