Na Mwandishi Wetu.
CHAMA cha Wafanyakazi wa Vyombo vya Habari Tanzania (JOWUTA) kesho kinatarajia kupokea ugeni kutoka Chama cha Waandishi wa Habari cha Oman (Omani Journalists Association – OJA), unaotarajiwa kuwasili nchini leo, Jumanne, Agosti 18, 2026.
Taarifa kuhusu ujio wa ugeni huo imetolewa na Katibu Mkuu wa JOWUTA, Selemani Msuya, ambaye amesema chama hicho kimeuchukulia kwa uzito ugeni huo kutokana na umuhimu wake katika kuimarisha ushirikiano wa kitaaluma.
Msuya alisema ugeni huo wa wajumbe wanne kutoka Oman unalenga kuimarisha mahusiano kati ya JOWUTA na OJA katika nyanja mbalimbali, ikiwemo eneo la taaluma ya uandishi wa habari.
“Ugeni huo unakuja nchini ikiwa ni sehemu ya kuimarisha mahusiano na JOWUTA katika nyanja mbalimbali, ikiwemo eneo la kitaaluma,” alisema Msuya.
Alisema wakati wa ziara hiyo, wajumbe hao watakutana na viongozi wa JOWUTA ambapo miongoni mwa mambo yatakayojadiliwa ni maandalizi ya kongamano litakalojulikana kama Oman–Tanzania Journalists Forum.
Aidha, alisema viongozi hao watajadili namna ya kuimarisha ushirikiano baina ya JOWUTA na OJA, pamoja na kuanzisha programu za kubadilishana uzoefu na maarifa miongoni mwa waandishi wa habari kutoka Tanzania na Oman.
Kwa mujibu wa Msuya, ugeni huo pia unatarajiwa kukutana na viongozi wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo pamoja na Wizara ya Maliasili na Utalii, kabla ya kuelekea Zanzibar baadaye.
Ziara hiyo inatarajiwa kuwa fursa ya kuimarisha uhusiano wa kitaaluma na kubadilishana uzoefu kati ya wanahabari wa Tanzania na Oman.

Hakuna maoni: