🔴🔴 KWA NINI KIPANDE KIDOGO CHA NYAMAPORI KINAWEZA KUSABABISHA ADHABU KUBWA?



📍Je, wakati sisi tunakiona kipande, Sheria inaona nini?!!

✍️ Na Beatus Maganja

Kila mara taarifa zinapotolewa kuhusu mtu aliyekamatwa akiwa na kipande cha nyama ya mnyamapori, ngozi, jino au nyara nyingine, mijadala huibuka mitandaoni. Wapo wanaouliza kwa mshangao, "Inawezekanaje mtu afungwe miaka mingi kwa sababu ya kipande kidogo tu?" Wengine hufikia hatua ya kuiita Sheria ya Uhifadhi wa Wanyamapori kuwa kandamizi. Lakini je, tumewahi kusimama na kujiuliza kwa nini sheria imeweka msimamo huo?

Pengine tatizo si ukali wa sheria, bali namna tunavyolitazama kosa lenyewe. Mara nyingi macho yetu huona ukubwa au udogo wa kipande kilichokamatwa, lakini sheria hutazama chanzo cha kipande hicho. *Swali la msingi huwa si, "Ni kikubwa kiasi gani?" bali, "Kimepatikanaje?"*

Hebu fikiria kwa mfano jino la tembo. Halijipeleki lenyewe sokoni, wala halidondoki lenyewe kutoka kwa tembo aliye hai Ili lipatikane, mara nyingi kuna tembo aliyepoteza maisha au nyara iliyochukuliwa kinyume cha sheria. Hivyo, kipande kidogo kinakuwa ushahidi wa mnyororo mpana zaidi wa uhalifu dhidi ya rasilimali za Taifa.

Sheria nyingi duniani zinazohusu ujangili au uhalifu mkubwa hazitazami uzito wa kitu pekee, bali madhara ya kitendo. Ndiyo maana, katika baadhi ya makosa, hata kiasi kidogo cha kitu kinachohusishwa na uhalifu kinaweza kuwa na athari kubwa za kisheria. Mantiki hiyo ndiyo inayotumika pia katika mapambano dhidi ya ujangili au biashara haramu ya nyara za wanyamapori.

Wapo wanaosema, "Lakini huyu alikuwa na kipande kidogo tu." Ni hoja inayostahili kusikilizwa. Hata hivyo, ikiwa sheria ingeruhusu kila mtu kuwa na "kipande kidogo", je, ni vipande vingapi vingekusanywa baada ya mwezi mmoja, mwaka mmoja au miaka mitano? Je, soko la biashara haramu lisingeendelea kukua kwa kujificha nyuma ya hoja ya "kidogo tu"? Wakati mwingine, njia bora ya kuzuia ujangili mkubwa ni kukata mianya yake midogo.

Tusisahau kwamba wanyamapori si mali ya mtu mmoja. Ni urithi wa Watanzania wote na wa vizazi vijavyo. Tembo, faru, simba, chui na wanyamapori wengine wameifanya Tanzania ijulikane duniani, wamechangia ukuaji wa utalii, wamezalisha ajira na mapato ya fedha za kigeni na wameifanya nchi yetu kuwa miongoni mwa mataifa yenye bioanuwai ya kipekee. Kila nyara inayopatikana kinyume cha sheria ni pigo kwa urithi huo.

Hii ndiyo sababu sheria haikulenga tu kumwadhibu anayekamatwa. Lengo lake kubwa ni kutuma ujumbe kwa jamii kwamba biashara haramu ya nyara haikubaliki kwa namna yoyote. Sheria inalinda mnyama ambaye hawezi kujitetea na inalinda maslahi ya Taifa ambayo mara nyingi hayaonekani kwa macho ya haraka.

Ni muhimu pia kutambua kwamba mahakama hutoa maamuzi kwa kuzingatia sheria, ushahidi uliowasilishwa na mazingira ya kila kesi. Hivyo, si sahihi kudhani kwamba kila mtu anayekutwa na nyara hupata adhabu inayofanana. Kila shauri husikilizwa kwa misingi yake na kwa mujibu wa sheria husika.

Badala ya kuuliza kwa nini adhabu ni kubwa, pengine tuanze kuuliza swali lingine muhimu zaidi..*Kwa nini nyara hizo zilikuwa mikononi mwa mtu bila uhalali?* Tukipata jibu la swali hilo, huenda tukaelewa kwa nini sheria imeamua kulinda rasilimali hizi kwa nguvu kubwa kiasi hicho.

Mwisho wa yote, lengo la Sheria ya Uhifadhi wa Wanyamapori si kujaza magereza. Lengo lake ni kulinda rasilimali hizi Kwa ajili ya kikazi chetu na vizazi vijavyo ili viendelee kurithi Tanzania yenye utajiri wa wanyamapori kama tulivyorithi sisi leo.

Elimu ndiyo silaha bora kuliko adhabu. Kadiri jamii inavyoelewa thamani ya rasilimali za wanyamapori na mantiki ya sheria zinazozilinda, ndivyo tunavyojenga ushirikiano mkubwa zaidi katika uhifadhi. Na pale wananchi wanapokuwa washirika wa uhifadhi ndipo Taifa lote hunufaika.

Hakuna maoni:

Inaendeshwa na Blogger.