Muleba, Kagera
Mradi wa Kituo cha Kuongeza Msukumo wa Mafuta (Pump Station 3 – PS3) katika Mradi wa Bomba la Mafuta Ghafi la Afrika Mashariki (EACOP), kilichopo Wilaya ya Muleba mkoani Kagera, umefikia asilimia 88 ya utekelezaji na unatarajiwa kukamilika mwishoni mwa Agosti au mwanzoni mwa Septemba mwaka huu.
Hayo yameelezwa Agosti 7, 2026 na Mkurugenzi wa Mipango na Uwekezaji wa Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC), Bw. Derick Moshi, wakati wa ziara ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa kituo hicho.
Bw. Moshi amesema PS3 ni kituo cha tatu katika mradi wa EACOP kuanzia Uganda na cha kwanza upande wa Tanzania. Amefafanua kuwa kazi zote kuu za ujenzi zimekamilika na kinachoendelea ni kazi za ukamilishaji pamoja na majaribio ya mifumo kabla ya kituo kuanza kufanya kazi.
Aidha, amesema mradi huo umekuwa shamba darasa kutokana na ushirikiano mzuri kati ya Serikali na sekta binafsi katika utekelezaji wake, jambo lililowezesha kubadilishana ujuzi, kujenga uwezo wa wataalamu wa ndani na kuimarisha ushirikiano katika miradi mikubwa ya kimkakati.
Ameongeza kuwa mradi huo unaendana na Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 kwa kuimarisha ushiriki wa sekta binafsi katika maendeleo ya sekta ya nishati na kuendeleza miundombinu ya kisasa. Pia amesema kukamilika kwa PS3 kutachangia usafirishaji salama na wenye ufanisi wa mafuta ghafi kutoka Uganda kupitia Tanzania, hatua itakayochochea ukuaji wa uchumi na kuongeza nafasi ya Tanzania kama kitovu cha miundombinu ya nishati katika ukanda wa Afrika Mashariki.
Kwa upande wake, Kiongozi wa Timu ya Mkandarasi wa Kituo hicho, Dmitry Malyshev, amesema ameridhishwa na ziara ya wataalamu kutoka Wizara ya Nishati na TPDC kwani imewapa fursa ya kupokea maoni na maelekezo ya kitaalamu yatakayosaidia kukamilisha mradi kwa ubora, usalama na kwa kuzingatia viwango vinavyohitajika.








Hakuna maoni: