Na Mwandishi Wetu,
Dar es Salaam.
SERIKALI imewataka wamiliki na waendeshaji wa Miundombinu Muhimu ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) nchini kuhakikisha miundombinu hiyo inasajiliwa kwa mujibu wa sheria, hatua inayolenga kuimarisha ulinzi wa mifumo ya kidijitali na usalama wa taifa.
Wito huo umetolewa na Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Bi Anjela Kairuki wakati akieleza kuwa usajili huo ni sehemu ya juhudi za Serikali kuhakikisha mifumo na miundombinu ambayo ina umuhimu mkubwa kwa uchumi na huduma za jamii inalindwa dhidi ya mashambulizi ya kimtandao na vihatarishi vingine.
Alisema hatua hiyo inatekelezwa kwa mujibu wa Kifungu cha 28(1) cha Sheria ya Makosa ya Mtandao ya mwaka 2015, kinachompa Waziri mwenye dhamana ya mawasiliano mamlaka ya kutangaza na kusimamia Miundombinu Muhimu ya TEHAMA.
Kwa mujibu wa maelezo hayo, miundombinu hiyo inahusisha mali, vifaa, mifumo ya kompyuta na mitandao, iwe inayoonekana au isiyoonekana, ambayo ina umuhimu mkubwa kwa taifa kiasi kwamba kuharibika au kusimama kwa huduma zake kunaweza kusababisha madhara makubwa kwa usalama, uchumi na ustawi wa jamii.
Sekta zinazohusishwa na miundombinu hiyo ni pamoja na habari na mawasiliano, fedha na benki, maji, afya, nishati na madini, usafirishaji, chakula na kilimo, ujenzi, uchumi wa buluu, mazingira, viwanda, ulinzi na anga.
Sekta nyingine ni elimu, utawala wa kiraia, ulinzi wa raia, ardhi pamoja na maeneo yanayohusisha usalama na utulivu wa umma.
Serikali ilitangaza rasmi miundombinu hiyo kupitia Tangazo la Serikali Na. 147 la Juni 19, 2024, ambapo wamiliki na waendeshaji walipewa muda wa miezi sita, kuanzia tarehe hiyo hadi Desemba 19, 2024, kukamilisha usajili.
Katika hatua nyingine, Serikali imeandaa miongozo mitano kwa kushirikiana na wadau kutoka sekta ya umma na binafsi Tanzania Bara na Zanzibar, kwa lengo la kuwezesha usimamizi bora wa miundombinu hiyo.
Miongozo hiyo inahusu utambuzi na usimamizi wa Miundombinu Muhimu ya TEHAMA, ukaguzi, tathmini ya vihatarishi, uadilifu na uhalisia wa data pamoja na mipango ya kurejesha huduma baada ya kutokea majanga.
Usajili wa miundombinu hiyo unafanyika kwa njia ya mtandao kupitia Mfumo wa Usajili wa CII (CII Portal), huku wamiliki wakitakiwa kufungua akaunti na kuwasilisha taarifa zinazohitajika kuhusu miundombinu yao.
Serikali pia imeweka njia za mawasiliano kwa ajili ya kutoa msaada na kujibu maswali ya kiufundi, ikiwamo namba za simu 0612 600 600, 0612 400 400 na 0733 124 972, pamoja na barua pepe support.ciiregistry@mawasiliano.go.tz.
Aidha, wamiliki na waendeshaji wa miundombinu hiyo wanatakiwa kutoa taarifa kwa mamlaka husika ndani ya saa 24 endapo kutatokea tukio la kiusalama, shambulio au changamoto nyingine inayoweza kuathiri utendaji wa miundombinu husika.
Serikali imeonya kuwa mtu atakayebainika kuharibu au kuingilia miundombinu hiyo anaweza kuchukuliwa hatua kwa mujibu wa Kifungu cha 29 cha Sheria ya Makosa ya Mtandao ya mwaka 2015.
Adhabu zinazoweza kutolewa ni pamoja na faini isiyopungua Sh milioni 100, kulipa mara tatu ya thamani ya hasara iliyosababishwa, kifungo kisichopungua miaka mitano au adhabu zote mbili kwa pamoja.
Waziri amewataka wadau wote kushirikiana na Serikali katika kuhakikisha miundombinu hiyo inalindwa, akisisitiza kuwa usalama wa mifumo hiyo ni muhimu katika kulinda uchumi wa kidijitali, huduma muhimu za jamii na usalama wa taifa kwa ujumla.







Hakuna maoni: