Na Herry Kilele,
Dodoma
Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Utafiti wa Uvuvi Tanzania (TAFIRI), Dkt. Ismael A. Kimirei, amesema Taasisi hiyo imejipanga kikamilifu kutumia Maonesho ya Nanenane Kitaifa 2026 kuwaelimisha wananchi kuhusu teknolojia mbalimbali zilizobuniwa kupitia tafiti za uvuvi na ukuzaji viumbe maji.
Akizungumza na waandishi wa habari Agosti 1, 2026, katika Viwanja vya Dkt. John Samwel Malecela, Nzuguni, Jijini Dodoma, Dkt. Kimirei amesema ushiriki wa TAFIRI katika maonesho hayo ni fursa muhimu ya kuwafikia wananchi na wadau mbalimbali wa Sekta ya Uvuvi na ukuzaji viumbe maji.
Amesema kupitia maonesho hayo, TAFIRI inatoa elimu na taarifa sahihi zinazotokana na utafiti wa kisayansi kwa wananchi, wadau wa Sekta ya Uvuvi na ukuzaji viumbe maji, wanafunzi, watafiti na makundi mbalimbali ya jamii.
"Lengo letu ni kuendelea kuelimisha umma kuhusu umuhimu wa utafiti wa uvuvi na ukuzaji viumbe maji, pamoja na kuonesha matokeo ya tafiti, teknolojia na bunifu mbalimbali zinazolenga kuchangia maendeleo ya Sekta ya Uvuvi na Uchumi wa Buluu nchini Tanzania," amesema Dkt. Kimirei.
Aidha, amesema TAFIRI itaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali kuhakikisha matokeo ya tafiti yanafika kwa watumiaji na kuchangia katika maendeleo ya Sekta ya Uvuvi Nchini.
Dkt. Kimirei amewakaribisha wananchi na wadau kutembelea Banda la TAFIRI katika Maonesho ya Nanenane 2026, ambapo watapata fursa ya kujifunza kuhusu teknolojia mbalimbali zilizobuniwa na Taasisi hiyo, ikiwemo teknolojia ya kutotoresha vifaranga vya sato inayohamishika, inayolenga kurahisisha upatikanaji wa vifaranga bora kwa ajili ya shughuli za ukuzaji viumbe maji.
Amesema wananchi wanaotembelea banda hilo pia watapata fursa ya kujifunza zaidi kuhusu tafiti, teknolojia na bunifu mbalimbali zinazolenga kuendeleza Sekta ya Uvuvi na tasnia ya ukuzaji viumbe maji nchini Tanzania.

Hakuna maoni: