TFRA YASAJILI AINA 65 ZA MBOLEA HAI KUONGEZA UPATIKANAJI WA PEMBEJEO SALAMA

Na Mwandishi Wetu, 

Dodoma.

Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA) imesajili jumla ya aina 65 za mbolea za asili, maarufu kama mbolea hai, katika hatua inayolenga kuongeza upatikanaji wa pembejeo salama, bora na rafiki kwa mazingira kwa wakulima nchini.

Hayo yameelezwa na Meneja wa Usajili na Leseni wa TFRA, Mwahija Irika, wakati akizungumza katika mjadala kuhusu kilimo ikolojia uliofanyika katika Ukumbi wa Midahalo wa Wizara ya Kilimo, Viwanja vya Nane Nane, jijini Dodoma.

Irika amesema kanuni zilizowekwa na mamlaka zimeendelea kujenga mazingira wezeshi kwa wazalishaji wa mbolea kuwekeza na kusajili bidhaa zao, huku TFRA ikiendelea kuwapa ushirikiano katika mchakato huo.

"Tumefanikiwa kusajili aina 65 za mbolea za asili. Aidha, kuna wazalishaji zaidi ya 15 wa mbolea hai ambao wametambulika rasmi na kuingizwa katika mfumo wa udhibiti wa mamlaka," amesema.

Amesema TFRA itaendelea kusajili mbolea zote zinazokidhi vigezo vilivyowekwa ili kuhakikisha wakulima wanapata mbolea hai kwa urahisi na bila kukumbwa na changamoto ya upatikanaji wake.

Irika ameongeza kuwa mamlaka inaendelea kutoa elimu kwa wakulima kuhusu matumizi sahihi ya mbolea, akisisitiza kuwa mbolea za asili na za viwandani zinapaswa kutumika kwa kukamilishana kupitia mfumo wa Usimamizi Jumuishi wa Rutuba ya Udongo, unaolenga kuboresha afya ya udongo na kuongeza tija ya uzalishaji.

Amesema juhudi hizo zinaungwa mkono na Serikali ambayo imeendelea kutambua mchango wa mbolea hai katika kujenga mifumo endelevu ya uzalishaji wa chakula na kulinda mazingira.

Pia amebainisha kuwa katika hotuba ya bajeti ya Wizara ya Kilimo, Waziri wa Kilimo, Daniel Chongolo, alisisitiza umuhimu wa kuhamasisha uzalishaji na matumizi ya mbolea hai nchini.

Kwa upande mwingine, Irika amesema Serikali ina mpango wa kushirikiana na halmashauri zote nchini kuhamasisha matumizi ya mabaki ya mazao pamoja na taka nyingine zinazoweza kuchakatwa ili kuzalisha mbolea za asili, hatua itakayosaidia kuongeza uzalishaji wa ndani na kupunguza utegemezi wa mbolea kutoka nje ya nchi.

Hakuna maoni:

Inaendeshwa na Blogger.