TTCL KINARA HUDUMA BORA ZA MAWASILIANO

DAR ES SALAAM

Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL) limeongoza kwa ubora wa huduma za mawasiliano nchini baada ya kufikisha kiwango cha asilimia 98 katika kipimo cha ubora wa huduma (Quality of Service).

Matokeo hayo yametajwa katika ripoti iliyowasilishwa na Waziri wa Mawasiliano, huku TTCL ikieleza kuwa mafanikio hayo yametokana na maboresho makubwa yaliyofanyika katika miundombinu na mifumo ya utoaji huduma kwa wateja.

Akizungumza kuhusu matokeo hayo, Meneja Mahusiano wa TTCL, Esther Mbanguka, amesema shirika hilo limefurahishwa na matokeo hayo, akieleza kuwa ni matokeo ya uwekezaji unaoendelea kufanyika katika miundombinu ya mawasiliano na mifumo ya huduma.

Amesema TTCL imeendelea kuboresha miundombinu pamoja na mifumo ya ndani na nje inayolenga kurahisisha upatikanaji wa huduma kwa wateja na kuongeza ufanisi wa utoaji wa huduma.

«“TTCL imekuwa kinara katika utoaji wa huduma bora za mawasiliano. Haya yote yanawezekana kutokana na miundombinu ambayo tumeiboresha zaidi, lakini pia uwekezaji katika mifumo ya ndani na mifumo ya nje ya namna ya kuwahudumia wateja wetu kwa urahisi na unafuu zaidi,” amesema Mbanguka.»

Mbanguka amesema TTCL itaendelea kuwekeza na kuboresha miundombinu yake ili kuhakikisha huduma za mawasiliano zinawafikia wananchi katika maeneo mbalimbali nchini.

Ameongeza kuwa maboresho yataendelea pia katika mifumo ya huduma kwa wateja, huku shirika likilenga kuhakikisha mifumo inayosaidia utoaji wa huduma inawekwa na kukamilishwa kwa wakati.

Kwa mujibu wa TTCL, hatua hizo zinalenga kuimarisha ufanisi wa huduma na kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora, rahisi na zenye kukidhi mahitaji yao.

Hakuna maoni:

Inaendeshwa na Blogger.