USAFIRISHAJI HARAMU WA BINADAMU WACHUKUA SURA MPYA, VIJANA WATEKWA MTANDAONI


Na Mwandishi Wetu,

Dar es Salaam. 

DAR ES SALAAM

Wadau wa mapambano dhidi ya usafirishaji haramu wa binadamu wameitaka Serikali, vyombo vya ulinzi na usalama pamoja na jamii kuongeza juhudi za kukabiliana na uhalifu huo ambao sasa umeanza kutumia teknolojia na mitandao ya kijamii kuwatega na kuwateka waathirika.

Wito huo umetolewa katika mdahalo wa kitaifa uliowakutanisha wadau kutoka serikalini, mashirika ya kimataifa, taasisi za dini na mashirika yasiyo ya kiserikali, kwa lengo la kutathmini hali ya usafirishaji haramu wa binadamu nchini na kuweka mikakati ya pamoja ya kukabiliana nao.

Mkurugenzi wa Mtandao wa Kitaifa wa Kuzuia Usafirishaji Haramu wa Binadamu na Afisa Mtendaji Mkuu wa Tanzania Relief Initiatives (TRI), Edwin Mugambila, alisema mdahalo huo unalenga kukusanya maoni ya wataalamu na wadau mbalimbali ili kuweka mikakati thabiti ya kukabiliana na tatizo hilo.

Alisema usafirishaji haramu wa binadamu unaathiri moja kwa moja ajenda za maendeleo ya taifa, ikiwemo utekelezaji wa Dira ya Maendeleo 2050, utawala bora, ulinzi wa haki za binadamu na ujenzi wa jamii yenye amani na usalama.

Mugambila alisema tatizo hilo linaendelea kujitokeza kwa sura mbalimbali, ikiwemo ajira za shuruti katika mashamba na migodi, unyonyaji wa majumbani, biashara ya ngono pamoja na biashara haramu ya viungo vya binadamu.

Alisema Kanda ya Mashariki, inayojumuisha Dar es Salaam, Morogoro na Pwani, imeonekana kuwa miongoni mwa maeneo yenye matukio mengi, huku Kanda ya Ziwa nayo ikishuhudia ongezeko la matukio hayo.

“Baadhi ya mikoa inakuwa chanzo cha waathirika, mingine inatumika kama njia ya kupitisha waathirika na mingine kuwa maeneo ya mwisho wanakopelekwa,” alisema.

Aidha, Mugambila alisema teknolojia na mitandao ya intaneti vimeanza kutumiwa na wahalifu kama njia ya kuwavuta na kuwateka vijana, ambapo baadhi yao hushawishiwa kwa ahadi za ajira au fursa mbalimbali kabla ya kuishia kulazimishwa kufanya vitendo vya uhalifu.

Alisema baadhi ya waathirika hufungiwa katika nyumba na kulazimishwa kufanya utapeli mtandaoni au kuwashawishi watu wengine kujiunga na mitandao hiyo ya uhalifu.

Kutokana na hali hiyo, alizitaka Serikali, vyombo vya upelelezi na jamii kuongeza umakini, kutoa taarifa mapema na kuhakikisha watuhumiwa wanakamatwa na kufikishwa mahakamani ili sheria ichukue mkondo wake.

Kwa upande wake, Mwakilishi wa Hanns Seidel Foundation nchini Tanzania, Frank Olvitzer, alisema usafirishaji haramu wa binadamu umekuwepo kwa muda mrefu, lakini kwa miaka mingi haukupewa mwanga na utafiti wa kutosha.

Alisema ripoti mpya iliyoandaliwa kwa ushirikiano na Tanzania Relief Initiatives imeanza kuweka wazi ukubwa wa tatizo hilo kwa kutoa takwimu na ushahidi unaoweza kusaidia Serikali na wadau kupanga hatua madhubuti za kukabiliana nalo.

Olvitzer alisema tofauti na baadhi ya maeneo ya Ulaya ambako usafirishaji haramu wa binadamu mara nyingi huhusisha kuvuka mipaka ya nchi, barani Afrika tatizo hilo linahusisha zaidi usafirishaji wa ndani ya nchi pamoja na ule wa kimataifa.

Alisema umaskini na ukosefu wa fursa za kiuchumi ni miongoni mwa sababu zinazowafanya baadhi ya watu kuwa katika mazingira hatarishi ya kutekwa na kusafirishwa.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Carage Worldwide Tanzania, Susan James Shaw, alisema nyumba salama zinazoendeshwa na taasisi hiyo katika miji ya Moshi na Dar es Salaam zinaendelea kutoa huduma kwa watoto na wanawake waliokumbwa na ukatili na usafirishaji haramu wa binadamu.

Alisema waathirika hupatiwa hifadhi salama, ushauri nasaha wa kisaikolojia pamoja na msaada wa kisheria ili kuwasaidia kurejea katika maisha ya kawaida wakati taratibu za kisheria dhidi ya watuhumiwa zikiendelea.

Wadau hao kwa pamoja wamewataka wazazi, viongozi wa serikali za mitaa na jamii kwa ujumla kuongeza uangalizi kwa watoto na vijana, hususan matumizi yao ya mitandao ya kijamii, na kutoa taarifa kwa mamlaka pindi wanapobaini viashiria vya usafirishaji haramu wa binadamu.

Hakuna maoni:

Inaendeshwa na Blogger.