WAZIRI KAIRUKI:- UBORA WA HUDUMA ZA MAWASILIANO WAONGEZEKA, UTAPELI WAPUNGUA

DAR ES SALAAM: 

Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Angellah Jasmine Mbelwa Kairuki, amesema ubora wa huduma za mawasiliano nchini umeendelea kuimarika, huku matukio ya utapeli wa mitandao yakipungua kwa asilimia 25.29 katika robo mwaka iliyoishia Juni 2026.

Waziri Kairuki ameyasema hayo leo, Agosti 10, 2026, wakati akizungumza na waandishi wa habari katika mkutano uliofanyika Makao Makuu ya Mamlaka ya Udhibiti wa Mawasiliano Tanzania (TCRA), jijini Dar es Salaam, kuhusu Ripoti ya Hali ya Sekta ya Mawasiliano ya Robo mwaka kuanzia mwezi machi hadi Juni 2026.

Amesema ripoti hiyo imeonyesha mafanikio katika maeneo mbalimbali ya sekta hiyo, ikiwemo kuongezeka kwa ubora wa huduma za simu, ukuaji wa matumizi ya intaneti na huduma za fedha mtandao, pamoja na kupungua kwa matukio ya ulaghai yanayotumia mitandao ya mawasiliano.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, kiwango cha ufikiwaji wa vigezo vya kisheria vya ubora wa huduma za simu kimeongezeka kutoka asilimia 94.3 katika robo ya Januari hadi Machi 2026 hadi kufikia asilimia 96.4 katika robo iliyoishia Juni, sawa na ongezeko la asilimia 2.1.

Tathmini hiyo ilifanyika katika mikoa na maeneo 22 nchini kwa kuhusisha mitandao ya Vodacom, Yas (Tigo), Airtel, Halotel na TTCL.

Hata hivyo, Waziri Kairuki amesema bado kuna maeneo ambayo yanahitaji maboresho ya huduma, huku kampuni za simu zikitakiwa kuchukua hatua za haraka katika maeneo yaliyobainika kuwa na ubora hafifu.

Maeneo hayo ni pamoja na Dodoma, Geita, Kagera, Katavi, Kigoma, Pemba na Unguja, Tabora na Rukwa, pamoja na wilaya za Ubungo na Kigamboni jijini Dar es Salaam.

Katika hatua nyingine, Waziri Kairuki amesema matukio ya ulaghai yaliyoripotiwa katika robo ya Aprili hadi Juni 2026 yamepungua kwa asilimia 25.29, kutoka matukio 9,817 katika robo iliyotangulia hadi kiwango cha chini katika robo hiyo.

Amesema TCRA imebaini jumla ya laini za simu 7,334 zilizohusishwa na matukio ya ulaghai, huku kupungua kwa matukio hayo kukihusishwa na msako na ukaguzi wa pamoja uliofanywa na TCRA kwa kushirikiana na vyombo vya ulinzi na usalama katika mikoa ya Dar es Salaam, Arusha, Mbeya na Mara.

Amesema serikali kupitia TCRA itaendelea kushirikiana na wadau wa sekta hiyo pamoja na vyombo vya ulinzi na usalama katika kukabiliana na vitendo vya utapeli wa mitandao.

“Wananchi wanapaswa kuwa makini kwa kutotoa namba zao za siri, OTP wala taarifa binafsi kwa watu wasioaminika, na wanapaswa kuepuka kubofya viunganishi visivyojulikana,” amesema.

Ameongeza kuwa wananchi wanaweza kuripoti namba zinazohusishwa na vitendo vya utapeli kwa kutuma namba hiyo kwenda 15040 kupitia ujumbe mfupi wa simu, ili hatua stahiki zichukuliwe.

Kuhusu huduma za posta, ripoti hiyo imeonyesha bidhaa za kiposta zilizopokelewa kutoka nje ya nchi zimeongezeka kwa asilimia 52.2, kutoka 44,555 mwezi Machi hadi 67,800 mwezi Juni 2026.

Kwa upande mwingine, bidhaa za kiposta zilizotumwa ndani ya nchi zimepungua kwa asilimia 9.9, kutoka 546,644 mwezi Machi hadi 492,335 mwezi Juni, hali ambayo imeelezwa kuchangiwa na kuongezeka kwa matumizi ya barua pepe na huduma za jumbe za papo kwa papo kama WhatsApp.

Aidha, Waziri Kairuki amesema matumizi ya huduma za mawasiliano yanaendelea kukua nchini, ambapo laini za simu hai zimefikia milioni 117, watumiaji wa intaneti milioni 62.79, watumiaji wa simu janja milioni 31.34 na akaunti za pesa mtandao milioni 87.05.

Amesema upatikanaji wa huduma ya mtandao wa 5G umeongezeka kutoka asilimia sifuri mwaka 2021 hadi kufikia asilimia 4.4, hatua inayokwenda sambamba na utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo ya Mwaka 2050 na mipango ya mabadiliko ya kidijitali nchini.

Waziri Kairuki amesema serikali itaendelea kufuatilia mwenendo wa sekta ya mawasiliano na kutoa taarifa za maendeleo yake kwa umma kupitia takwimu za kila robo mwaka, kwa lengo la kuongeza uwazi na uwajibikaji katika sekta hiyo.

Hakuna maoni:

Inaendeshwa na Blogger.