ACT WAZALENDO WAITAKA SERIKALI KUCHUKUA HATUA KUKABILIANA MADHARA YA MVUA

Dar es Salaam. 

Chama cha ACT Wazalendo kimeitaka Serikali kuchukua hatua za haraka na za vitendo kukabiliana na madhara yanayoweza kusababishwa na mvua, kikisisitiza kuwa wananchi hawahitaji maneno ya kisiasa bali maandalizi madhubuti ya kuwalinda.

Wito huo umetolewa na Waziri Mkuu Kivuli wa ACT Wazalendo, Isihaka Mchinjita, ambaye amesema uwezekano wa mvua kubwa unaweza kusababisha madhara kwa wananchi endapo Serikali haitachukua hatua za maandalizi mapema.

Mchinjita amesema Serikali inapaswa kuunda Timu Maalumu ya Kitaifa ya Kukabiliana na Majanga, itakayohusisha Ofisi ya Waziri Mkuu, Ofisi ya Rais–TAMISEMI na Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), kwa lengo la kuratibu na kufuatilia maandalizi ya kukabiliana na majanga katika ngazi zote.

Amesema timu hiyo inapaswa kuhakikisha wizara, mikoa, wilaya na mamlaka za serikali za mitaa zinaweka mipango madhubuti ya kukabiliana na athari za mvua.

Aidha, ACT Wazalendo imeitaka Serikali kuongeza fedha kwa Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) ili kuwezesha ununuzi na uhifadhi wa chakula cha kutosha kwa ajili ya dharura na maeneo yatakayokumbwa na majanga.

Kwa mujibu wa Mchinjita, Serikali inapaswa kupunguza matumizi yasiyo ya lazima na ya anasa na kuelekeza rasilimali zaidi katika maandalizi ya majanga na ulinzi wa maisha ya wananchi.

Katika hatua nyingine, chama hicho kimezitaka mikoa na wilaya kutambua na kutangaza mapema maeneo yaliyo katika hatari ya mafuriko na majanga mengine yanayoweza kusababishwa na mvua.

Mchinjita amesema mamlaka hizo zinapaswa pia kuandaa maeneo salama ya kuwahamishia wananchi endapo hali itakuwa mbaya, huku elimu ya tahadhari ikitolewa kwa wananchi, wakulima, wafugaji na wavuvi kwa kushirikiana na vyombo vya habari na asasi za kiraia.

Kuhusu miundombinu, ACT Wazalendo imeitaka Serikali kuharakisha ujenzi na ukarabati wa madaraja, makaravati na barabara, pamoja na kusafisha na kupanua mitaro na njia za maji ili kupunguza hatari ya mafuriko.

Mchinjita amesema miradi ya miundombinu iliyo katika maeneo hatarishi inapaswa kukamilishwa kwa haraka au kufikia kiwango salama kabla ya mvua kuanza.


Maeneo ya migodi

ACT Wazalendo pia imesisitiza umuhimu wa kuchukua hatua maalumu katika maeneo yenye shughuli za uchimbaji madini.

Mchinjita amesema shughuli za uchimbaji zinapaswa kusitishwa kwa muda katika maeneo yatakayobainika kuwa hatarishi, huku wamiliki wa migodi wakitakiwa kuimarisha kingo na kutengeneza njia salama za maji ili kuzuia mafuriko na ajali.

Amesema hatua hizo ni muhimu hasa katika maeneo ambayo shughuli za uchimbaji zinaweza kuongeza hatari kwa maisha ya wachimbaji na wananchi wanaoishi jirani na migodi.


Afya na uokoaji

Katika eneo la afya na uokoaji, ACT Wazalendo imeitaka Serikali kuongeza wataalamu, dawa na vifaa tiba, pamoja na kuandaa kambi za dharura katika maeneo yanayoweza kuathirika.

Mchinjita amesema uwezo wa uokoaji nao unapaswa kuimarishwa kwa kuweka tayari helikopta, boti, jaketi za kujiokoa na zana nyingine muhimu za uokoaji.

Amesema vyombo vya ulinzi na usalama vinapaswa kushirikishwa kikamilifu katika maandalizi hayo ili kuhakikisha Serikali ina uwezo wa kutoa msaada wa haraka pale majanga yanapotokea.

Kwa upande wa uongozi, ACT Wazalendo imewataka viongozi wa ngazi zote kuwa kazini kikamilifu, hususan katika maeneo yaliyoainishwa kuwa hatarishi, badala ya kusubiri majanga yatokee ndipo hatua zichukuliwe.

Mchinjita pia ameitaka Serikali kutoa taarifa na elimu endelevu kwa umma kuhusu tahadhari zinazopaswa kuchukuliwa kabla na wakati wa mvua.

“Hatutaki maneno bila vitendo,” amesema Mchinjita, akisisitiza kuwa maandalizi ya mapema yanaweza kusaidia kuokoa maisha, kulinda mali na kupunguza madhara yanayoweza kujitokeza kutokana na mvua.



Hakuna maoni:

Inaendeshwa na Blogger.