BENKI Kuu ya Tanzania (BoT) imewasihi wasanii na washereheshaji nchini kutumia ushawishi wao kwa jamii kuhamasisha wananchi kutunza na kutumia kwa usahihi noti na sarafu, ikieleza kuwa utunzaji wa fedha ni jukumu la kila mmoja.
Rai hiyo imetolewa leo jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi wa Tafiti na Uchumi wa BoT, Dkt. Suleiman Misango, wakati akifungua semina maalum iliyowakutanisha wasanii na washereheshaji mbalimbali nchini.
Aidha,Dkt. Misango amesema, ushiriki wa wasanii katika kuelimisha jamii kuhusu matumizi na utunzaji sahihi wa fedha ni muhimu kutokana na nafasi yao kubwa katika jamii na uwezo wao wa kufikisha ujumbe kwa hadhira pana.
Dkt. Misango amesema, wananchi wanapaswa kuelewa kuwa namna wanavyoshughulikia noti na sarafu ina mchango mkubwa katika kuhakikisha fedha hizo zinadumu katika mzunguko na kupunguza gharama zinazotokan kuzibadilisha mara kwa mara.
Hata hivyo, Dkt. Misango,amesema noti zilizochakaa au kuhalibika zinaweza kusababisha changamoto katika utendaji wa baadhi ya mashine za ATM, hali inayoweza kuongeza gharama za uendeshaji na matengenezo kwa watoa huduma za kifedha.
"Hizi fedha, noti na sarafu usipozitunza vizuri, hata kwenye mashine hasa za ATM hazitoki vizuri, bila kujua kuwa unamuongezea gharama mtoa huduma wa fedha,benki. Hivyo, mwisho wa siku mnaweza kugawana gharama za kuhudumia mashine," amesema.
Amesema suala la utunzaji wa fedha halipaswi kuangaliwa kama jukumu la Benki Kuu pekee, bali ni wajibu unaohitaji ushirikiano wa wananchi, taasisi za fedha na wadau wengine, wakiwemo wasanii wenye ushawishi mkubwa katika jamii.
BoT imewaelimisha kuhusu shughuli za kifedha zinazohitaji leseni, na madhara ya vitendo vya kukusanya amana kutoka kwa wananchi na kutoa mikopo bila kuwa na leseni kutoka Benki Kuu ya Tanzania.

Hakuna maoni: