DCEA YAKAMATA KILO 18,078 ZA DAWA ZA KULEVYA, YABAINI MAGARI YA MISIBA YATUMIKA KUSAFIRISHA MIHADARATI

Dar es Salaam. 

Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) imekamata jumla ya kilogramu 18,078.41 za dawa za kulevya katika operesheni zilizofanyika katika mikoa 14 nchini kuanzia Julai hadi Septemba 2026.

Akizungumza na Waandishi wa habari wakati akaitoa taarifa ya operesheni hiyo Kamishina Jenerali wa Mamlaka ya Kupambana na Dawa za Kulevya DCEA Aretas Lyimo , amesema kiasi hicho kinajumuisha kilogramu 11,504.76 za bangi, kilogramu 6,529.5 za mirungi, kilogramu 44.45 za bangi aina ya skanka na gramu 41.25 za heroin, huku jumla ya watuhumiwa 289 wakikamatwa na 169 kati yao kufikishwa mahakamani.

Mamlaka pia imebaini kuwa magari yanayosafirisha miili ya marehemu kwenda kwenye misiba mikoani yanatumiwa na baadhi ya wafanyabiashara haramu kusafirisha dawa za kulevya, hususan mirungi, skanka na bangi.

Kamishina Lymo ameongeza kuwa, matumizi hayo yameonekana zaidi katika Ukanda wa Kaskazini, ikiwemo Moshi, Kilimanjaro, Arusha na Tanga, ambapo baadhi ya magari yanayosafirisha miili yanadaiwa kutumika kubeba dawa hizo wakati yanakwenda au yanaporudi kutoka kwenye misiba.

Kutokana na taarifa za kiintelijensia zilizokusanywa, Mamlaka imeeleza kuwa itaanza kufanya ukaguzi maalum wa magari yanayosafirisha miili, pale yatakapokuwa na viashiria au kutiliwa shaka kuwa yanatumika kusafirisha dawa za kulevya.

Mamlaka imeonya kuwa iwapo gari la msiba litakamatwa likiwa limebeba dawa za kulevya na mhusika au mmiliki wa dawa hizo asipatikane, watu wote waliomo ndani ya gari hilo wanaweza kukamatwa na kuchukuliwa hatua za kisheria, wakiwemo ndugu wa marehemu, abiria na dereva.

DCEA imewataka ndugu na familia zinazokodi magari kwa ajili ya kusafirisha miili ya wapendwa wao kuwa makini na kuhakikisha wanakagua na kujiridhisha kuhusu mizigo yote inayoingizwa kwenye magari hayo kabla ya kuanza safari, ili kuepuka kuhusishwa na makosa ya jinai.

Katika operesheni hizo, DCEA pia ilikamata magari nane, bajaji moja na pikipiki 40 zilizohusishwa na tuhuma za usafirishaji wa dawa za kulevya, huku ikiendelea kuwataka wamiliki na waendeshaji wa vyombo vya usafiri kuimarisha udhibiti wa mizigo na usimamizi wa wafanyakazi.

Aidha, Mamlaka imebaini matumizi ya mabasi ya abiria katika usafirishaji wa mirungi, ambapo katika tukio moja watuhumiwa walikamatwa wakisafirisha bando 238 za mirungi zenye uzito wa kilogramu 125.33 kwa kutumia basi la RATCO lililokuwa likisafiri kati ya Tanga na Dar es Salaam.

Kamishina Lymo ameendelea kutoa wito kwa wananchi kutoa taarifa kuhusu watu wanaojihusisha na biashara na usafirishaji wa dawa za kulevya, pamoja na wale wanaotumia nafasi hiyo kujihusisha na vitendo vya rushwa na uhalifu.

Hakuna maoni:

Inaendeshwa na Blogger.