KHEA YAFIKIA WAWEZESHAJI 360, WAKULIMA 1500+ KILIMO IKOLOJIA HAI


Mradi wa kilimo ikolojia hai unaotambulika kwa jina la Kitovu cha Maarifa cha Afrika Mashariki (KHEA), umefikia tamati Septemba 30, 2026, baada ya kuwawezesha wawezeshaji 360 ambao kwa pamoja wamewafikia wakulima zaidi ya 1,500 na kuwapatia elimu na mbinu mbalimbali za kilimo ikolojia hai.

Mradi huo umewafikia wawezeshaji kutoka maeneo mbalimbali Tanzania Bara, yakiwemo Njombe, Kilimanjaro, Songwe na Mtwara, pamoja na Zanzibar, huku wawezeshaji hao wakipeleka elimu waliyoipata kwa wakulima katika maeneo yao.

Akizungumza wakati wa hafla ya kufunga mradi huo, Msimamizi wa Miradi wa Taasisi ya Kilimo Hai Tanzania (TOAM), Brigita Didas, amesema kukamilika kwa mradi huo kunatoa fursa kwa wanufaika kuendelea kutumia elimu na mbinu za kilimo ikolojia hai walizojifunza wakati wa utekelezaji wa mradi.

Amesema lengo kuu la mradi huo ni kukusanya na kusambaza maarifa ya kilimo ikolojia hai katika ngazi ya Afrika Mashariki, ikiwemo kuyaweka katika mifumo ya kidijitali ili yaweze kuwafikia na kunufaisha wadau katika nchi nyingine.

Didas amesema mradi huo umetumia mbinu rahisi za kufikisha elimu kwa wanufaika, ikiwemo kuwahamasisha kutumia malighafi zinazopatikana katika mazingira yao kutengeneza pembejeo muhimu kama vile mbolea na viuatilifu vya kilimo ikolojia hai.

Kwa upande wao, wanufaika wa mradi huo kutoka Zanzibar, waliowakilisha wawezeshaji kutoka maeneo mengine, wameeleza kuwa mradi huo umefungua fursa na kuongeza uelewa kuhusu kilimo ikolojia hai.

Mmoja wa wawezeshaji hao, Salama Hussein Makame, amesema ametumia elimu aliyopata kuwafundisha wakulima namna ya kutengeneza viuatilifu vya kilimo ikolojia hai kwa kutumia malighafi zinazopatikana katika mazingira yao, ikiwemo miti dawa.

Amesema matumizi ya miti dawa inayopatikana katika maeneo ya wakulima yamerahisisha utekelezaji wa kilimo hicho, huku yakisaidia kupunguza gharama za kununua viuatilifu vya kilimo hai.

Mradi huo pia umefundisha mbinu mbalimbali za kilimo ikolojia hai, ikiwemo uzalishaji wa bidhaa za kilimo hai zenye ubora, namna ya kufikia masoko na uwezeshaji wa makundi rika.

KHEA ni mradi unaohusisha nchi za Tanzania, Uganda, Rwanda, Kenya na Madagascar, ukiwa na lengo la kuimarisha ukusanyaji, usambazaji na matumizi ya maarifa ya kilimo ikolojia hai katika ukanda wa Afrika Mashariki.

Hakuna maoni:

Inaendeshwa na Blogger.