ZANZIBAR.
TAASISI ya Permaculture Practical Institute Zanzibar (PPIZ) imetangaza kuzindua hivi karibuni kampeni maalum ya lishe inayolenga watoto na mama wajawazito, kwa kutumia njia za kilimo endelevu na chakula salama.
Kampeni hiyo itatekelezwa Unguja na Pemba kwa ushirikiano kati ya PPIZ, UNICEF, Milele Zanzibar Foundation na Mwambao, ikiwa ni sehemu ya programu ya pamoja ya kuboresha lishe ya watoto Zanzibar.
Hayo yamesemwa na Mkurugenzi Mkuu wa PPIZ, Ikram Ramadhan Soraga, katika siku maalum ya afya, ulaji na lishe ndani ya Tamasha la Kilimo Hai Zanzibar (ZOF) linaloendelea Dole Kizimbani.
"Awali yote namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutujaalia kuwa hapa leo katika siku ya tamasha letu la kilimo hai. Leo ni siku mahususi kwa masuala ya afya ya ulaji na lishe, na tunakushukuru sana Mheshimiwa Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Hamad Omar Bakari kwa kuja kuungana nasi na kutuzindulia kampeni yetu," amesema Soraga.
Amesema Kampeni hiyo imelenga Kaskazini Unguja, Magharibi A na Kaskazini Pemba ikihusisha zaidi lishe ya watoto na mama mjamzito kuanzia maandalizi ya chakula nyumbani.
"Tuna programu ya pamoja na ndugu zetu UNICEF ya kuboresha lishe ya watoto kwa kutumia mbinu za kilimo endelevu. Programu hii tutaifanya Unguja na Pemba. Kwa upande wetu PPIZ tutakuwa Kaskazini Unguja na Wilaya ya Magharibi A, na kwa upande wa Pemba tutakuwa Kaskazini Pemba," alifafanua.
Aliongeza kuwa katika utekelezaji huo, wenzao wa Milele Zanzibar Foundation na Mwambao pia wanatekeleza kwa maeneo yao.
"Tumejikita kwenye lishe ya mtoto na mama mjamzito. Tumeamua kuanza na namna ya waandaaji wa chakula. Kwenye hadhara hii ya leo utaona mama zetu na wazazi wapo humu ndani, ni muhimu sana wao wafahamu namna ya kuandaa chakula salama na chenye lishe.
Tunaamini lishe bora inaanzia shambani. Tukihakikisha chakula kinazalishwa kwa njia endelevu na mama anajua namna sahihi ya kukitayarisha, tunalinda afya ya mtoto na mama yake." amesema Soraga.
Akifungua siku hiyo maalum Naibu Waziri wa Fedha na Mipango Zanzibar, Dk Hamad Omar, amesema kaulimbiu ya "Tufikiri Kiulimwengu, Tule Kiasili" ndio mwelekeo wa serikali katika kujenga uchumi unaozingatia afya, mazingira na usalama wa chakula.
Akizungumza katika siku ya maonesho ya upishi ya "Pika na Mama Mariam" ndani ya Tamasha la Kilimo Hai, Omar ambaye alimwakilisha Mama Mariam Mwinyi, alisema kilimo hai na kilimo ikolojia ni sehemu muhimu ya mustakabali wa maendeleo ya Zanzibar.
Naibu Waziri alisema Mpango Mkakati wa Kisekta wa Lishe Zanzibar unaonyesha kuwa takriban mtoto 1 kati ya watoto 10 wenye umri wa miezi 6 hadi 23 pekee ndiye anayepata vyakula kutoka angalau makundi matano ya chakula.
"Mara nyingi tatizo sio ukosefu wa chakula, bali ni uelewa wa jinsi ya kuchanganya na kupika tulivyonavyo. Leo tutaona jinsi mazao ya ndani kama mchicha, maboga, viazi vitamu, kunde, samaki, mayai na matunda yanavyoweza kuandaliwa nyumbani kuwa chakula cha mtoto chenye virutubisho kwa gharama nafuu," alisema.
Alipongeza PPIZ chini ya Mkurugenzi wake Ikram kwa kuongoza juhudi za kuwapatia wakulima maarifa na kuwaunganisha na masoko, na ZMBF kwa kuwa mdau muhimu wa lishe kupitia programu za malezi ya awali ya mtoto.
Omar alisema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imejidhatiti kutokomeza utapiamlo kupitia utekelezaji wa Mpango Mkakati wa Kisekta wa Lishe 2024/25 - 2028/29.
"Tumepiga hatua udumavu kwa watoto chini ya miaka mitano umeshuka kutoka asilimia 24 mwaka 2015/16 hadi asilimia 17.6 mwaka 2022, na lengo letu ni kuufikisha asilimia 11.6 ifikapo 2028/29," alibainisha.
Alisema juhudi hizo zinaenda sambamba na dhamira ya Rais Dk Hussein Ali Mwinyi ya kuwawezesha wakulima kuongeza uzalishaji kwa gharama nafuu huku wakihifadhi rutuba na vyanzo vya maji, ndiyo maana serikali imezindua Mkakati wa Kilimo Hai.
"Kama Waziri mwenye dhamana ya Fedha nahakikishia kuwa serikali itaendelea kuweka mazingira wezeshi na kutenga rasilimali kwa programu hizi. Kama tulivyojenga barabara na bandari, tunapaswa pia kujenga miundombinu ya akili kupitia lishe bora," alisema.
Alitolea mfano Jimbo lake la Micheweni Pemba ambalo lilikuwa na changamoto kubwa ya upungufu wa damu kwa mama wajawazito na watoto, sasa zaidi ya akina mama 16,000 wamefikiwa na elimu ya lishe na hali zao zimeimarika.
"Tulishangaa, sisi ni watu wa bahari, tunapata samaki wa kutosha, kwa nini tupate changamoto ya lishe? Kumbe ni suala la uelewa wa namna ya kuandaa vyakula vya lishe. Elimu hii imewasaidia sana," alisema.
Alieleza kuwa kilimo hai kinajenga udongo wenye rutuba, kinalinda vyanzo vya maji, bahari ambayo ni tegemeo kwa wavuvi, wakulima wa mwani na utalii, na kinatupatia chakula salama chenye mabaki machache ya kemikali - jambo muhimu zaidi kwa watoto wadogo.
Mtaalamu wa Lishe kutoka Shirika la Umoja wa Mataifa linalohudumia Watoto (UNICEF), Hawa Msola, amesema juhudi za kuhamasisha lishe bora kwa watoto na familia lazima ziende sambamba na kuhakikisha chakula kinachozalishwa ni salama.
Msola alishukuru waandaaji wa tamasha hilo, akisema jukwaa hilo limekuwa muhimu kwa kuliunganisha suala la lishe, afya, kilimo na mifugo.
"Wageni waalikwa, tunafahamu lishe bora inaanza na upatikanaji wa chakula cha aina mbalimbali chenye virutubisho na kilicho salama. Tunapohamasisha watoto na familia kula mboga, matunda na vyakula vingine, ni muhimu pia kuzingatia jinsi vinavyozalishwa, vinavyohifadhiwa na vinavyoandaliwa," alisema.
Alisema maonesho ya kilimo hai na ya upishi yanayofanyika katika tamasha hilo yanatoa fursa ya kuona jinsi vyakula vinavyopatikana jamii vinaweza kuzalishwa kwa njia ya kilimo hai na kuchangia lishe bora, hasa kwa watoto.
"Maonesho haya ya upishi yanatusaidia kupeleka ujumbe karibu zaidi na familia kupitia kuonyesha namna vyakula vya mazingira yetu vinaweza kuandaliwa kuwa milo yenye virutubisho, salama na inayoweza kutekelezwa kila siku," aliongeza.
Msola alisisitiza kuwa kuboresha lishe kunahitaji ushirikiano wa sekta mbalimbali - serikali, wakulima, jamii, mashirika ya kiraia, sekta binafsi na washirika wa maendeleo - katika kujenga mifumo ya chakula inayowezesha upatikanaji wa chakula chenye virutubisho, salama na endelevu.
"UNICEF itaendelea kushirikiana kwa karibu na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na wadau kama PPIZ. Kwa pamoja tuhakikishe kila mtoto na kila familia inapata chakula chenye virutubisho, salama na kinachochangia afya na ustawi wake," alihitimisha.
Msaidizi wa Afisa Mtendaji Mkuu Shirika la Zanzibar Maisha Bora Foundation (ZMBF), Honest Nyamei limeitaja rasilimali ya mwani kama mkombozi mpya wa lishe bora kwa watoto na familia Zanzibar, ambayo bado haijatumiwa kikamilifu licha ya upatikanaji wake kwa wingi.
"Ni heshima kubwa kuwa pamoja nanyi katika tukio hili linalolenga kutoa elimu na kuimarisha lishe bora. Kwa niaba ya Afisa Mtendaji Mkuu na Mwenyekiti wetu, Mama Mariam Mwinyi, napenda kutambua juhudi zinazofanywa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na wadau katika kuboresha afya na lishe," alisema.
Nyamei alisema ZMBF inaamini lishe bora ndio msingi wa maisha bora - msingi wa afya, ukuaji, uwezo wa kujifunza na ustawi wa familia.
"Lishe haipaswi kuangaliwa kama suala la kiafya pekee, bali kama sehemu muhimu ya ajenda pana ya maendeleo ya Zanzibar. Mwili unahitaji mchanganyiko wa virutubisho ili ukue na kujikinga na magonjwa," alisema.
Katika muktadha huo, alisema moja ya rasilimali muhimu na rahisi inayopatikana Zanzibar ni mwani, ambao kwa muda mrefu umekuwa sehemu ya shughuli za kiuchumi, hususan kwa wanawake wanaoishi karibu na bahari.
"Mwani una uwezo wa kutumika katika ubunifu wa bidhaa mbalimbali za chakula, jambo ambalo watu wengi hawafahamu. Leo hapa kuna mama mmoja anaitwa Bissafia, ukipita kwenye meza yake utajifunza vitu vingi - kuna unga wa lishe, uji uliotengenezwa kwa mwani, snacks, na unaweza kutumika kama salad. Una virutubisho vingi vinavyosaidia ukuaji wa mtoto na familia nzima, na bei yake ni nafuu," alieleza.
Aliongeza kuwa miaka ya mwanzo ya maisha ya mtoto ni kipindi muhimu sana, ambapo lishe bora huchangia ukuaji wa mwili, maendeleo ya ubongo na kinga ya mwili.
"Mtoto anayepata lishe bora, malezi yenye upendo na mazingira salama, anawekewa msingi mzuri wa kufikia uwezo wake. Hili ni jukumu la familia nzima, jamii, serikali na wadau wote," alisema.
Alisisitiza kuwa elimu ya lishe inapaswa kuzingatia mazingira halisi ya familia, na kutumia mazao yanayopatikana kwa urahisi kama mwani.






Hakuna maoni: