RAIS MWINYI AAGIZA KUANZISHWA KITENGO CHA KILIMO HAI

ZANZIBAR:

Rais wa Zanzibar, Dk. Hussein Ali Mwinyi, ameiagiza Wizara ya Kilimo, Umwagiliaji, Maliasili na Mifugo kuanza mchakato wa kuanzisha Kitengo Maalum cha Kilimo Hai kitakachoratibu na kusimamia shughuli za kilimo hai visiwani humo.

Agizo hilo amelitoa Septemba 23, katika Viwanja vya Dole, wakati wa ufunguzi wa Tamasha la Kilimo Hai Zanzibar (Zanzibar Organic Festival), lenye kaulimbiu “Fikiri Kiulimwengu, Kula Kiasili”.

Akizungumza mbele ya wakulima, wafanyabiashara, wanafunzi na wageni kutoka mataifa mbalimbali, Rais Mwinyi amesema tamasha hilo limekuwa jukwaa muhimu tangu kuanzishwa kwake mwaka 2023 kwa ajili ya kubadilishana uzoefu, maarifa, teknolojia na ubunifu, pamoja na kukuza biashara ya mazao ya kilimo hai.

Amesema kilimo ni sekta muhimu katika uchumi wa Zanzibar na Serikali imeendelea kufanya mageuzi kwa kuwekeza katika teknolojia ya kisasa, miundombinu ya umwagiliaji, mikopo nafuu na upatikanaji wa masoko.

“Lengo letu ni kuwafanya wakulima wetu waongeze uzalishaji wa chakula kwa gharama nafuu huku wakihifadhi rutuba ya udongo, maji na kulinda afya za walaji. Hii ndiyo maana ya kilimo hai na kilimo ikolojia,” amesema.

Rais Mwinyi amesema Serikali imezindua Mkakati wa Kilimo Hai Zanzibar na kusisitiza kuwa utekelezaji wake unapaswa kuonekana katika shughuli za kilimo, bajeti, huduma za ugani, upatikanaji wa pembejeo, tafiti na mnyororo mzima wa thamani.

Aidha, ameiagiza Wizara hiyo kufanya tathmini ya uwezekano wa kuingiza pembejeo za kilimo hai katika mpango wa ruzuku ya pembejeo za kilimo ili kupunguza gharama kwa wakulima.

Amesema Serikali itaendelea kudhibiti matumizi yasiyodhibitiwa ya pembejeo za kemikali, huku ikitoa elimu kwa wakulima kuhusu matumizi salama na endelevu ya pembejeo.

Dk. Mwinyi amesema ukuaji wa sekta ya utalii Zanzibar, ambayo mwaka 2024 ilipokea zaidi ya watalii 600,000, unatoa fursa kubwa kwa wakulima kupitia mahitaji ya chakula salama na chenye viwango vya kimataifa.

Ametoa wito kwa hoteli, migahawa na waandaaji wa chakula kuongeza ununuzi wa mazao kutoka kwa wakulima wa Zanzibar, akisisitiza umuhimu wa kuimarisha mfumo wa “Shambani Hadi Mezani”.

Awali, Mwenyekiti wa tamasha hilo, Iqram Soraga, alimuomba Rais Mwinyi kuelekeza Wizara ya Kilimo, Umwagiliaji, Maliasili na Mifugo kuanzisha kitengo maalum cha kilimo hai na kutoa ruzuku kwa pembejeo za kilimo hicho.

Soraga amesema tamasha hilo limeendelea kupata mafanikio na kutoa fursa kwa wadau wa kilimo hai kubadilishana uzoefu na kuendeleza jitihada za kukuza kilimo ikolojia Zanzibar.

Amesema kuanzishwa kwa Mkakati wa Kilimo Hai Zanzibar kutasaidia kuongeza kasi ya jitihada hizo, huku akitaka utekelezaji wake ufanyike kwa vitendo.

Kwa upande wake, Mwakilishi wa Shirika la Island of Peace (IDP), Richard Libent, amesema ushiriki wao katika tamasha hilo umekuwa fursa ya kukuza biashara, kubadilishana uzoefu na kuongeza wigo wa masoko.

Amesema kupitia tamasha hilo wameweza kukutana na wadau mbalimbali wa kilimo ikolojia, wakiwemo Mwavuli wa Kilimo Hai Tanzania (TOAM) na wadau wengine wanaofanya shughuli zinazofanana.

“Kama mdau nimelipokea kwa furaha sana. Ndicho kitu tunachopigania, kwamba hata bidhaa za kiekolojia kama mbolea hai ziwekwe ruzuku kama mbolea nyingine ili wakulima na watumiaji waweze kuipata kwa urahisi,” amesema.

Richard amependekeza tamasha kama hilo kuandaliwa pia Tanzania Bara, akitaja miji ya Dodoma na Arusha, ili kuongeza ushirikiano na fursa kwa wakulima na wadau wa kilimo hai nchini.

Hakuna maoni:

Inaendeshwa na Blogger.