DAR ES SALAAM.
Ushirikiano wa kiutamaduni na utalii kati ya Tanzania na China unazidi kuimarika kupitia mabadilishano ya uzoefu, utangazaji wa vivutio na fursa za utalii, hatua inayolenga kuongeza uelewa na kuimarisha mahusiano kati ya wananchi wa nchi hizo mbili.
Akizungumza katika hafla ya kutangaza fursa za utalii na utamaduni wa Mkoa wa Guizhou nchini China, Jijini Dar es Salaam, Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi Ofisi kiunganishi TANAPA Dar es salaam, Neema Philippo Mollel, amesema utamaduni na utalii vinatoa fursa ya kujifunza, kuheshimiana na kujenga uhusiano wa karibu kati ya wananchi wa Tanzania na China.
Amesema Tanzania ina utajiri mkubwa wa utalii unaojumuisha hifadhi za taifa 21, zikiwemo Kilimanjaro, Serengeti, Tarangire na Ruaha, pamoja na maeneo ya kihistoria na kiakiolojia kama Kilwa Kivinje, Kilwa Kisiwani, Kondoa Irangi na Makumbusho ya Mwalimu Nyerere.
Amesema Guizhou ina utajiri mkubwa wa maliasili na utamaduni, ukiwemo milima, misitu na tamaduni za makabila zaidi ya 18, huku maboresho ya miundombinu ya usafiri na mazingira ya biashara yakifungua zaidi fursa za utalii na ushirikiano wa kimataifa.
Amesema Guizhou ina maeneo manne yaliyosajiliwa na UNESCO kama Urithi wa Asili wa Dunia, ambayo ni Libo, Shibing, Fanjingshan na Chishui, pamoja na vivutio vingine kama Maporomoko ya Maji ya Huangguoshu na Pango la Shuanghe lenye urefu wa zaidi ya kilomita 409.
Aidha, amesema mkoa huo una utajiri mkubwa wa tamaduni za makabila 18, ikiwemo nyimbo za jadi za makabila ya Dong na Miao, kazi za mikono kama urembo wa nguo wa Miao na mfumo wa kale wa maandishi wa Shui.
Katika hatua nyingine, Mtaalamu wa Kahawa kutoka Guizhou, Wang Xiaojia, ameeleza fursa ya ushirikiano katika sekta ya kahawa, akisema Guizhou imekuwa na ongezeko kubwa la matumizi ya kahawa licha ya kutokuwa mzalishaji mkubwa wa mbegu hizo.
Amesema mji wa Guiyang una zaidi ya maduka na migahawa 3,000 ya kahawa, huku utamaduni huo ukikua kwa kasi kutokana na historia ya wakazi wa Guizhou kuthamini vinywaji vyenye ladha mbalimbali.
Wang amehimiza ushirikiano wa kibiashara utakaoifanya kahawa ghafi na bora kutoka Tanzania kupata soko la moja kwa moja katika Mkoa wa Guizhou, huku akitaja fursa zinazoweza kunufaisha wazalishaji na wafanyabiashara wa nchi hizo mbili.
TANAPA pamoja na wadau wengine wameeleza utayari wa kuendelea kushirikiana na China katika kukuza utalii endelevu, uhifadhi wa mazingira na kubadilishana uzoefu wa kiteknolojia na kitaalamu kwa lengo la kuimarisha sekta ya utalii kwa manufaa ya vizazi vya sasa na vijavyo.










Hakuna maoni: