TANZANIA YATANGAZA FURSA 150 ZA MASOMO YA SAYANSI NCHINI ALGERIA

DAR ES SALAAM.

Serikali kupitia Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia imetangaza fursa za ufadhili wa masomo nchini Algeria kwa wanafunzi 150 waliofanya vizuri katika masomo ya Sayansi kwenye mitihani ya Kidato cha Sita.

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda, amesemafursa hizo zimetokana na ushirikiano kati ya Tanzania na Algeria, ambapo Serikali ya Algeria italipia ada za masomo huku Serikali ya Tanzania kupitia Samia Scholarship ikigharamia mahitaji ya kujikimu.

Amesema uteuzi wa wanafunzi hao utafanyika kwa kuzingatia ufaulu bila kujali uwezo wa kifedha wa familia, hatua inayolenga kuwapa nafasi wanafunzi wenye uwezo kutoka familia za kawaida, wakiwemo watoto wa wakulima na wafugaji.

Waziri Mkenda amesema wanafunzi watakaokwenda Algeria watapewa mafunzo ya Kifaransa kwa mwaka mmoja kabla ya kuanza masomo, huku wanafunzi watakaokataa nafasi wakibadilishwa na wanaofuata kwa ufaulu.

Ameongeza kuwa Serikali tayari imewapatia wanafunzi 10 fursa ya kusoma nchini Urusi, huku wengine 50 waliofanya vizuri katika Advanced Mathematics wakipelekwa Nelson Mandela Institute, Arusha, kwa maandalizi ya masomo ya nje mwakani.

Profesa Mkenda amewataka wanafunzi waliofanya vizuri katika masomo ya Sayansi kufuatilia taarifa kupitia tovuti ya Wizara na kuhakikisha simu zao zinapatikana, huku Serikali ikiendelea na mazungumzo na nchi nyingine ili kuongeza fursa za masomo ya Sayansi na Hisabati nje ya nchi. 

Hakuna maoni:

Inaendeshwa na Blogger.