Zanzibar.
MKURUGENZI Mtendaji wa Mwamvuli wa Kilimo Hai Tanzania (TOAM), Bakari Mongo, amefafanua chanzo, malengo na utekelezaji wa Mkakati wa Taifa wa Kilimo Hai na Kilimo Ikolojia, akisema uamuzi wa kuwa na mkakati badala ya sera ulikuwa wa kimkakati ili kuepuka mchakato wa Bunge.
Akizungumza katika Tamasha la Kilimo Hai Zanzibar, Mongo alisema mkakati huo umetokana na maazimio ya wadau ya mwaka 2019 na makubaliano ya kitaifa na kimataifa kuhusu mabadiliko ya tabianchi na maendeleo endelevu.
"Watu wameanza kuelewa masuala ya kiafya na lishe, hasa katika makuzi ya awali ya mtoto. Kila mtu sasa anataka kujua bidhaa imezalishwa kwa mtindo upi, kwa kemikali au la. Ndiyo maana serikali zetu zimechukua hatua za makusudi kuondoa viwatilifu hatarishi," alisema.
Aliongeza kuwa Tanzania ni mwanachama wa mikataba mbalimbali ya kimataifa ya tabianchi na mpango kabambe wa maendeleo ya kilimo barani Afrika. Mwaka 2011, Umoja wa Afrika ulikubaliana kuanzisha programu ya kilimo hai katika nchi zote za Afrika Mashariki, ambapo TOAM ndio ilikuwa mratibu kwa Tanzania.
Kwa nini Mkakati na sio Sera?
Mongo alisema wazo la awali lilikuwa kuwa na sera, lakini wataalamu wa serikali walishauri kuwa sera ya kilimo iliyopo tayari ina vipengele vinavyounga mkono kilimo hai.
"Tulikuwa tunawaza kuwa na sera (policy), lakini wakasema hapana. Sera iliyopo inaonyesha vipengele vinavyosapoti kilimo hai, ni bora mkatengeze mkakati. Kwangu naona ni uamuzi sahihi. Sera unahitaji sheria na kanuni zipitishwe na Bunge, mchakato mrefu. Mkakati unatekelezeka haraka. Hata Zanzibar imefanya uamuzi sahihi kwa kuchagua mkakati," alifafanua.
Malengo 12, Vipaumbele sita
Alisema mkakati una malengo 12 yaliyofupishwa katika vipaumbele 6 vikuu ambapo mosi ni pembejeo hai.
"Huwezi kumwambia mkulima alime kilimo hai kama hana pembejeo. Nashukuru kupitia Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA), imesajili mbolea hai 63, lakini bado mahitaji ni makubwa. Wazalishaji wengi bado ni wadogo, tunatamani wazalishe kwa kiwango kikubwa."
Pili ni Huduma za Ugani ambapo kwa sasa wataalamu wengi wa kilimo (Bwana/Bibi Shamba) wamesoma kilimo cha kutumia kemikali na taasisi zao ndizo zinazoweka chachu, hivyo jitihada inahitajika ili wakulima wapate maarifa ya kilimo hai."
Kipaumbele ya tatu ni Masoko "Mkulima anazalisha lakini anahitaji kuuza. Lengo letu ni kuboresha soko la ndani na la Jumuiya ya Afrika Mashariki kwa kutumia mfumo wa PGS (Participatory Guarantee System). Sisi kama TOAM tuna mamlaka ya kudhibitisha kwa soko la ndani, tofauti na uthibitisho wa mtu wa tatu wa soko la nje."
Alitaja kipaumbele kingine ni Ardhi na kwamba mzalishaji wa kilimo hai anahitaji muda mrefu kujenga afya ya udongo. Asipokuwa na eneo la uhakika, akipangisha leo hapa kesho pale, inakuwa changamoto."
Pia uwekezaji kwenye mnyororo mzima wa thamani na kwamba mara nyingi tumejikita kusaidia wazalishaji tu. Tunawajengea uwezo wasindikaji, wasafirishaji, wauzaji na walaji ili mazao kutoka shambani mpaka kwa mlaji yawe salama."
Alisema pia Uratibu na Takwimu wamekuwa na mkakati, lakini wanahitaji kujua nani anafanya nini na wapi, na kutoa taarifa zenye takwimu zitakazoshawishi serikali kutenga bajeti.
Mongo alisema utekelezaji unafanywa na kiikosi kinachoongozwa na Wizara ya Kilimo, huku TOAM ikiwa sekretarieti.
"Mabadiliko ya kisera yanahitaji sauti ya wengi. Tutashawishi serikali kwa kutekeleza kikamilifu na kutoa takwimu zenye ushawishi. Mkakati bila utekelezaji na bila matokeo kwa wananchi hauna faida," alisisitiza.
Alimalizia kwa kupongeza Zanzibar kwa dhamira ya Rais ya kuanzisha Kitengo cha Kilimo Hai, na kusema mipango ijayo ni mikutano ya robo mwaka ya kikosi kazi, kuimarisha uratibu kizanda, na kuendelea kutafuta fedha kwa kuwa msaada wa wafadhili unapungua siku hadi siku.



Hakuna maoni: