WAFANYABIASHARA WATAKIWA KUIBUA MIRADI YA PPP


Pwani.

MKURUGENZI wa Kituo cha Ubia kati ya Sekta ya Umma na Binafsi (PPP Centre), David Kafulila, amewataka wafanyabiashara na wawekezaji kuacha kusubiri Serikali itangaze miradi ya PPP, bali waibue wenyewe fursa na kuwasilisha mapendekezo yao.

Kafulila amesema hayo leo Septemba 25, 2026, katika Kongamano la Fursa na Uwekezaji kuhusu PPP lililofanyika Kibaha, Mkoa wa Pwani.

Amesema hatua hiyo ni muhimu katika kufanikisha azma ya Tanzania kujenga uchumi wa dola trilioni moja kupitia sekta binafsi.

"Wawekezaji mjiandae, mtambue maeneo yenye fursa, mshirikiane na mamlaka za Serikali na mweleze nia yenu ya kuwekeza, bila kusubiri Serikali iandae mradi na kuutangaza," alisema.

Alisema Tanzania ina uwezo wa kufikia uchumi huo ambao nchi 21 tu duniani zimeufikia, lakini ni lazima kubadilisha fikra za Serikali na sekta binafsi.

Ameeleza kuwa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 si ya Serikali au Rais Samia pekee, bali ni ya Watanzania wote, na sekta binafsi ni mhimili muhimu wa utekelezaji wake.

"Kazi ya Mkurugenzi wa Halmashauri au Mkuu wa Wilaya sio kutawala watu tu. Ni kuwa-engage na kuwashirikisha katika biashara na uchumi," alisisitiza.

Aliutaja Mkoa wa Pwani kama eneo la kimkakati kwa uwekezaji na kuwataka wafanyabiashara kutumia fursa zilizopo kushirikiana na Serikali kuelekea malengo ya Dira 2050.

Hakuna maoni:

Inaendeshwa na Blogger.