WAKULIMA WASHAURI MBEGU ASILI ZIUZWE MADUKANI

WAKULIMA wanaolima kwa kufuata mbinu za kiikolojia wameishauri Serikali kuhakikisha maduka ya pembejeo za kilimo yanauza mbegu, mbolea na viuatilifu ambavyo vina sifa za kiikolojia.

Ushauri huo wameutoa jana mkoani Arusha wakati wa uzinduzi wa miradi mipya mitatu anbayo inaratibiwa na Shirika la Island of Peace (IDP) ambalo lilikuwa linaadhimisha mafanikio ya miradi ya Kilimo Endelevu Arusha+ na ECO-FOOD na kuzindua miradi mipya mitatu ambayo inaenda kuendeleza na kuwawezesha wakulima na kuimarisha mifumo endelevu ya chakula.

Uzinduzi huo umefanywa na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Arusha DC, Suleiman Msumi, ambapo alizindua miradi mipya mitatu ya Kilimo Endelevu Arusha+ II, ECO-FOOD II na SAFI Project, kwa lengo la kuendeleza kilimo ikolojia na lishe bora.

Mkulima Bakari Sumawe kutoka wilayani Karatu amesema miradi hiyo imewasukuma wakulima wengi kunufaika, hivvyo wanashauri kuwepo kwa mfumo rasmi wa usambazaji wa mbegu za asili ili mbegu hizo ziweze kupatikana kwa urahisi katika maduka ya pembejeo.

Sumawe amesema kwa sasa anawwza kuzalisha tani nyingi za mbegu asili, hivyo kinachohitaji ni kuhakikisha pembejeo hizo zinapatikana kila kona ya nchi.

Amesema mafanikio ambayo ameyapata kupitia miradi ya awali yamevutia wakulima katika kijiji chake kujifunza na kulima kwa mbinu za kiikolojia.

Bakari amesema mwitikio ambao umeoneshwa na wakulima kupitia elimu anayotoa ya upandaji na uhifadhi wa mbegu asili, unapaswa kuungwa mkono kwa kuwepo maduka yanayouza pembejeo hizo.

Naye Mkulima wa Mbogamboga, Flora Mollel kutoka kijiji cha Oldonyowas wilayani Arusha, amesema miaka mitatu ya miradi hiyo imebadilisha maisha yake na jamiii inayomzunguka, huku akisisitiza uwepo wa maduka pembejeo za asili ili kuendeleza kilimo ikolojia.

Flora amesema mwamko wawakulima kutumia pembejeo za asili ni mkubwa, hivyo ni wakati muafaka kwa serikali kuungana na wadau kama IDP, RECODA na Mtandao wa Vikundi vya Wakulima Mkoa wa Arusha (MVIWAARUSHA), ili kufikia wakulima wengi zaidi.

Adili Msangi amesema uendezwaji wa miradi hiyo unaenda kuleta mapinduzi makubwa kwenye mbegu na mbolea ambazo anazalisha.

Msangi amesema pembejeo asili zima faida nyingi, hivyo anaipongeza IDP kuamua kuendeleza miradi ambayo ina mrengo wa kiikolojia.

Aidha, wakulima na wazalishaji wa pembejeo za kilimo hao walitaja baadhi ya changamoto wanazopitia kuwa ni ukosefu wa masoko, ukosefu wa zana imara za kuzalisha pembejeo na nyingine.

Mkurugenzi wa IDP, Ayesiga Buberwa, amesema ECO-FOOD II italenga kuwawezesha wakulima na wajasiriamali katika usindikaji, kuongeza thamani na masoko ya bidhaa za kilimo ikolojia.

Amesema SAFI Project inalenga kutatua changamoto ya upatikanaji wa pembejeo hai, mashine na vifaa vidogo vya kilimo, ili kurahisisha kazi za wakulima, hususan wanawake.

Hakuna maoni:

Inaendeshwa na Blogger.