WANAWAKE WAPEWE NGUVU KUPITIA SANAA YA SARAKASI,WAONESHA UWEZO WAO


DAR ES SALAAM,

Mtandao wa Wasanii Wanawake nchini kwa kushirikiana na Chama cha Sarakasi Tanzania (TSA) pamoja na Makumbusho ya Taifa, umeendesha mradi wa kuwawezesha wasichana na wanawake kushiriki katika sanaa ya sarakasi na kupata fursa za kuonyesha vipaji vyao.

Mradi huo umejumuisha mafunzo na maonyesho yaliyofanyika kupitia programu ya Museum Art Explosion (MAE) katika Makumbusho ya Taifa na Nyumba ya Utamaduni jijini Dar es Salaam, ukiwa na lengo la kuongeza ushiriki wa wanawake katika sekta ya sanaa.

Wakizungumza katika maonyesho hayo, waandaaji wamesema mradi huo unalenga kuhakikisha wanawake na watoto wa kike wanapata nafasi ya kushiriki katika sanaa, uongozi na shughuli mbalimbali za kisanaa kwa usawa.

Dkt. Aloyce Mwambwiga, Mhifadhi kiongozi wa kituo Makumbusho ya Taifa na Nyumba ya Utamaduni jijini Dar es Salaam, amesema taasisi hiyo imeendelea kutoa jukwaa kwa wasanii na wabunifu kutumia kumbi zake kupitia programu ya MAYE, huku baadhi ya huduma zikitolewa bure au kwa gharama nafuu.

Amesema fursa hizo zinawezesha wasanii kuonyesha kazi zao, kuongeza ujuzi na kujenga nafasi zaidi za kiuchumi kupitia sanaa, huku akieleza kuwa Makumbusho ipo tayari kuwakaribisha wageni watakaofika nchini katika kipindi cha maandalizi na mashindano ya AFCON 2027.

Lizi Raphael, mmoja wa wasanii walioshiriki maonyesho hayo, amesema mafunzo waliyopata yamemjengea kujiamini na kumsaidia kutambua kuwa wanawake wanaweza kushiriki katika sanaa ya sarakasi kwa kiwango cha juu.
Coletta Benedict, ambaye pia alishiriki maonyesho hayo, amesema sanaa ya sarakasi imewafungulia wanawake fursa ya kutumia vipaji vyao kama chanzo cha ajira na kujikwamua kiuchumi.

Mratibu wa mradi wa Circus for Life, Habiba Issa, amesema pamoja na mafunzo ya sarakasi, washiriki wamepatiwa elimu kuhusu usalama kazini na usawa wa kijinsia ili kuwajengea uwezo wa kuendeleza vipaji vyao na kushiriki kikamilifu katika jamii.

Hakuna maoni:

Inaendeshwa na Blogger.